Simba, Yanga zaipasua kichwa Mashujaa
Muktasari:
- Mashujaa itaingia kwenye ratiba hiyo ikiwa na morali baada ya juzi, Alhamisi, kuichapa Polisi Tanzania mabao 2-1 katika kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
MECHI tatu zijazo za Ligi Kuu Bara zimekaa kimtego kwa Mashujaa FC, inayokabiliwa na mtihani wa kukutana na vigogo Simba, Azam FC na Yanga mfululizo huku kocha wake, Amani Josiah, akieleza namna watakavyoelekeza nguvu kwenye mandalizi ili kukabiliana na changamoto hiyo.
Mashujaa itaingia kwenye ratiba hiyo ikiwa na morali baada ya juzi, Alhamisi, kuichapa Polisi Tanzania mabao 2-1 katika kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Ushindi huo umeifanya timu hiyo kuendeleza rekodi yake nzuri ya nyumbani, ambako imeshinda mechi zote tatu ilizocheza kati ya saba na sasa wapo nafasi ya nne katika msimamo wa ligi.
Akizungumzia matokeo hayo na michezo inayofuata, Josiah amesema anafurahi kuona timu yake ikiendeleza ushindi inapocheza nyumbani, lakini anafahamu kuwa wanapaswa kujiandaa vizuri kwa sababu wapinzani wanaofuata wanahitaji umakini mkubwa.
“Nimefurahi kuona tumeendeleza rekodi nzuri nyumbani, sasa tunatakiwa kujiandaa na kuwa tayari kwa mechi hizo,” amesema.
Katika ratiba hiyo, Mashujaa itaanza kuivaa Simba (ugenini), Oktoba 13, 2026 kisha Oktoba 24, 2026 ikiwa na kibarua kingine Chamazi dhidi ya Azam kabla ya kurejea Kigoma, Oktoba 27, 2026 kucheza dhidi ya Yanga.
“Tunajua kwamba hizi ni mechi ngumu na tunapaswa kuzichukulia kwa uzito unaostahili. Kila mchezo una changamoto zake, kwa hiyo tunahitaji kujiandaa vizuri, kuwapa wachezaji maelekezo na kuhakikisha tunakuwa tayari tunapoingia uwanjani,” amesema kocha huyo.
Katika mechi saba zilizotajwa, timu hiyo imepata ushindi mara nne na kupoteza mara tatu, ikionyesha bado inahitaji kuimarika zaidi ili kufanya vizuri dhidi ya wapinzani wenye ushindani mkubwa.
Katika michezo yake ya nyumbani, mbali na kuichapa Polisi Tanzania pia ilitoa dozi kwa Singida Black Stars na Kagera Sugar kwa matokeo yanayofanana ya mabao 2-1.
Hata hivyo, vipigo vya ugenini ni dhidi ya Dodoma Jiji kwa bao 1-0 na Mbeya City kwa mabao 2-1, pamoja na kupoteza dhidi ya Fountain Gate kwa bao 1-0.