Fern Hawkins alivyoutuliza moyo wa Maguire
Muktasari:
- Fern ambaye amekuwa na uhusiano na Maguire kwa takribani miaka 15, aliamini kuwa mchezaji huyo alistahili kupata nafasi nyingine ya kucheza michuano hiyo, ambayo ilifanyika Marekani, Canada na Mexico.
BAADA ya Harry Maguire kuachwa katika kikosi cha England kwa ajili ya Kombe la Dunia 2026, moja ya watu waliochukizwa na uamuzi huo wa kocha Thomas Tuchel ni pamoja na mke wake, Fern Hawkins ambaye anatupa upande wa pili wa mchezaji huyo.
Fern ambaye amekuwa na uhusiano na Maguire kwa takribani miaka 15, aliamini kuwa mchezaji huyo alistahili kupata nafasi nyingine ya kucheza michuano hiyo, ambayo ilifanyika Marekani, Canada na Mexico.
"Nimevunjika moyo sana kwa ajili yako, hakuna na jambo lingine ambalo ungeweza kulifanya ili kuthibitisha ubora wako. Sina haja ya kukuambia jinsi unavyoheshimiwa, ila ni aibu kwamba ulikuwa unashindana na mtazamo wa mtu mmoja (Thomas Tuchel)," alisema Fern.
Kauli ya Fern ilionyesha kuwa ni mtu ambaye anapenda mafanikio ya mume wake na yupo tayari kuyapigania, kitu ambacho amekifanya kwa miaka mingi kabla hata Maguire hajajiunga na Manchester United.
Kama ambavyo wachezaji wengine hupitia panda shuka za uwanjani, ndivyo ilivyo na kwa Maguire ila jambo zuri kwake ni kwamba mara zote Fern amekuwa pembeni yake katika kipindi hicho hadi nyakati nzuri zitakaporejea tena.
Wawili hao ambao wanatokea katika eneo moja, Sheffield nchini England, wamekuwa pamoja tangu Juni 2011, huku ndoa yao ambayo ilifungwa huko Ufaransa ikijaliwa kupata watoto wawili hadi sasa.
Fern ni msomi wa Sayansi akiwa na shahada ya tiba ya viungo (Physiotherapy), ambayo aliihitimu mwaka 2017 lakini kwa sasa amejikita katika biashara zake binafsi ambazo hazihusiani na taaluma yake.
Akiwa kama mke na mama wa familia, bado Fern amekuwa akitenga muda wake na hata kusafiri kwenda kushuhudia mechi za mumewe. Mara kadhaa ameonekana akimshangilia Maguire akiwa uwanjani, iwe anachezea Man United au timu ya taifa ya England.
Maguire alimchumbia Fern hapo Februari 17, 2018, wakiwa jijini Paris, Ufaransa ambapo walienda kwa ajili ya mapumziko yao. Baada ya tukio hilo, Fern kupitia Instagram alisema kwamba Maguire amemfanya kuwa mwanamke mwenye furaha zaidi duniani.
Wakati wa Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, Fern alionekana akiwa amevaa pete yake ya uchumba huku akimsapoti Maguire pamoja na England. Kila England ipocheza alionekana uwanjani, na baada ya mechi walipiga pamoja picha ambazo zilipostiwa kwa wengi mtandaoni.
Mtoto wao wa kwanza, Lillie Saint alizaliwa hapo Aprili 2019, ikiwa ni miezi tisa baada ya England kuifunga Colombia kwa mikwaju ya penalti katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia la 2018.
Ikumbukwe baada ya ushindi huo, Maguire na Fern walipiga moja ya picha zao maarufu mtandaoni. Kufikia Mei 2020, Fern alijifungua mtoto wao wa pili ambaye walipewa jina la Piper Rose.
Hatimaye wawili hao walifunga ndoa 2022 ikiwa ni baada ya kuwa kwenye uhusiano kwa takribani miaka 11. Harusi yao iliyofanyika Ufaransa, ilihudhuriwa na mastaa mbalimbali akiwemo Jack Grealish na Jordan Pickford.
Kisha walielekea Amalfi Coast nchini Italia kwa ajili ya honeymoon (fungate) ambapo walionekana wakitumia muda wao katika fukwe za eneo hilo. Maguire aliitaja siku ya harusi yake kama siku ambayo hataweza kuisahau katika maisha yake.
Hivyo Maguire na Fern walifunga ndoa baada ya kupata watoto wao wawili, na hata katika picha za harusi yao, watoto wote wameonekana. Fern amekuwa akitumia ukurasa wake wa Instagram kuwaonyesha mashabiki sehemu ya maisha ya familia yao.
Mwaka mmoja baada ya ndoa, Fern alianzisha biashara yake ya maua inayojulikana kama Saint Rose. Jina hilo lilitokana na majina ya watoto wao wawili, Lillie Saint na Piper Rose. Biashara hiyo imejikita kutoa huduma za maua kwenye harusi na sherehe mbalimbali zikiwemo za mastaa.
Familia hiyo kwa sasa inaishi huko Cheshire katika jumba la kifahari lenye thamani ya takribani Pauni 4 milioni, wastani wa Sh14 bilioni. Ni nyumba yenye mandhari ya kuvutia ndani hadi nje ambapo ina eneo kubwa la wazi.
Kwa mujibu wa mtandao wa The Sun, nyumba hiyo ipo katika eneo la kifahari la Greater Manchester, karibu na maeneo walipoishi baadhi ya wachezaji wenzake wa zamani wa Man United, akiwemo Jesse Lingard na David De Gea ambaye sasa anaichezea Fiorentina.