Fungua pochi, Glazers wanasubiri ofa zenu
Muktasari:
- Mjasiriamali huyo kutoka Finland, amesema anapanga kuzungumza na wawekezaji mbalimbali kwa lengo la kuungana nao ili kuinunua timu hiyo.
MANCHESTER, ENGLAND: TAJIRI ambaye aliwahi kujaribu kuinunua Manchester United, Thomas Zilliacus amefunguka kuwa wamiliki wa timu hiyo, familia ya Glazer, kwa sasa wako tayari kuiuza.
Mjasiriamali huyo kutoka Finland, amesema anapanga kuzungumza na wawekezaji mbalimbali kwa lengo la kuungana nao ili kuinunua timu hiyo.
Zilliacus alikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kabisa kuonyesha nia ya kuinunua Man United wakati Glazers walipotangaza kuiuza Novemba 2022.
Hata hivyo, hakufanikiwa na badala yake bilionea Sir Jim Ratcliffe akanunua hisa za asilimia 30 kupitia kampuni yake ya Ineos.
Wiki hii, tetesi za Man United kuuzwa zilipamba moto baada ya afisa wa serikali ya Saudi Arabia, Turki Alalshikh, kudokeza klabu hiyo ipo kwenye mazungumzo ya uwezekano wa kununuliwa, jambo lililopingwa na baadhi ya vyanzo vya ndani kutoka kwa mashetani hao wekundu.
Lakini habari hizi zinaonekana kuwa na ukweli ndani yake kwani Zilliacus amethibitisha yeye pamoja na wawekezaji wengine wanajiandaa kuwasilisha ofa nono kwenda kwa familia ya Glazer ili kuinunua timu hiyo.
Akizungumza na gazeti la Manchester Evening News (MEN), Zilliacus amesema yupo katika mchakato wa mazungumzo na matajiri wengine kama Ratcliffe na Sheikh Jassim wa Qatar ili kuandaa ofa na kununua hisa za timu hizo zilizobakia kwa Glazers.
"Wiki iliyopita nilikuwa najiuliza njia bora ya kuinunua Man United na nikaandika mpango wa awali wa jinsi ya kuwafikia watu fulani kuona kama jambo hilo linaweza kufanyika. Lengo ni kuungana na watu sahihi ili kuirudisha Manchester United pale inapostahili kuwa."
Zilliacus, mwenye umri wa miaka 69, aliongeza hana tatizo kufanya kazi na wawekezaji wengine, hivyo atazungumza nao ili kuona kama watakuwa tayari kushirikiana katika mchakato huo.
"Sina tatizo kufanya kazi na watu kama Jim Ratcliffe au mwekezaji yeyote. Mimi siko hapa kwa ajili ya kujionyesha, bali kuijenga klabu ambayo nimekuwa nikiishabiki tangu nikiwa na miaka 12. Moyo wangu unaumia kuona hali ambayo timu inapitia kwa sasa. Man United ipo chini sana ikilinganishwa na pale ilipotakiwa kuwa. Mapenzi yangu kwa klabu hayajapotea. Nafikiri bado kuna nafasi yakuwa sehemu ya wamiliki. Ningependa sana kuzungumza na watu muhimu kuona nini kinaweza kufanyika."
Hata hivyo, Zilliacus mwenye utajiri wa takribani Dola 10 bilioni anasisitiza ni muhimu kwa timu hiyo kupata wawekezaji wanaoweka masilahi ya klabu mbele badala ya kutazama faida binafsi.
"Nilipoweka ofa yangu hapo awali, niligundua Glazers walikuwa wanacheza mchezo mchafu wa mimi, Ratcliffe na Sheikh Jassim kupandishiana dau. Nilisema hadharani huu ni ‘wenda wazimu’, kwa sababu fedha hizo walizokuwa wanazihitaji kutoka kwetu zingetumika kuboresha klabu ikiwa wangetuuzia kwa bei ya kawaida."
Kwa mtazamo wa tajiri huyu, Glazers wako tayari kuuza sehemu kubwa ya hisa zao kwani wameshapata fedha nyingi kama faida, tangu walipoinunua mwaka 2005.
"Hawana uhusiano mzuri na mashabiki na nafikiri hawatataka kuendelea kumiliki mali ambayo inawaletea lawama nyingi. Kwa hiyo naamini wakipata mtu atakayetoa dau sahihi, watataka kuuza na muda wa jambo hilo kutokea unaweza kuwa hivi karibuni," amesema Zilliacus ambaye pia kwa uzoefu wake amefunguka Glazars wanaweza kudai kiasi kikubwa sana cha pesa.