Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

FKF yashika hatma, kipigo cha mwamuzi wa mechi Sharks vs M.United

Muktasari:

  • Vurugu hizo zilizuka kwenye Uwanja wa Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi, wakati Sharks ikiwa mbele kwa mabao 2-1 na kufanya jumla ya mabao katika michezo miwili kuwa 3-3.

NAIROBI, KENYA. MECHI ya mchujo wa kupanda daraja kati ya Kariobangi Sharks na Mombasa United imevunjika kwa sababu ya ghasia za mashabiki, baada ya mwamuzi John Sulwe kuamua kuipatia Mombasa United penalti dakika ya 62.

Vurugu hizo zilizuka kwenye Uwanja wa Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi, wakati Sharks ikiwa mbele kwa mabao 2-1 na kufanya jumla ya mabao katika michezo miwili kuwa 3-3.

Baada ya uamuzi huo, wachezaji wa Sharks walimfuata mwamuzi wakilalamikia penalti hiyo, kabla ya mashabiki kuingia uwanjani na kumvamia Sulwe.

Mwamuzi huyo aliripotiwa kupigwa na mashabiki, huku walinzi wa uwanja pamoja na baadhi ya wanajeshi wa Kenya wakilazimika kuingilia kati na kumfikisha eneo salama.

Hata hivyo, vurugu ziliendelea kwa muda kabla ya polisi kuingia uwanjani na kuwaondoa mashabiki, waandishi wa habari na watu wengine waliokuwapo.

Mchezo huo ulikuwa wa marudiano wa mchujo wa kuwania nafasi ya kucheza Ligi Kuu ya Kenya msimu huu, baada ya Mombasa United kushinda mchezo wa kwanza kwa mabao 2-1 Alhamisi iliyopita kwenye Uwanja wa KPA Mbaraki Sports Club, Mombasa.

Mombasa United, iliyomaliza nafasi ya tatu katika National Super League msimu uliopita, ilianza kwa kasi na kufunga bao la kwanza dakika ya sita kupitia Jamal Messi, aliyefunga kwa kichwa kufuatia mpira wa kona.

Dakika ya 15, Mombasa ilikosa nafasi ya kuongeza bao baada ya Wakesho Jackson kushindwa kumalizia mpira uliokuwa umeachwa kufuatia krosi kutoka upande wa kushoto.

Sharks ilisawazisha dakika ya 25 kupitia nahodha Patillah Omotto kwa mpira wa adhabu, baada ya mshambuliaji Mohammed Hussein kuchezewa faulo nje kidogo ya eneo la penalti.

Dakika 10 baadaye, wenyeji walipata bao la pili kupitia Douglas Omanga, aliyefunga kwenye lango lililokuwa wazi baada ya kipa wa Mombasa, Williams Chigozie, kutoka golini kumfuata Eustace Chisala.

Kipindi cha pili, kocha wa Sharks, William Muluya, alifanya mabadiliko mawili kwa kuwatoa Omanga na Hussein na kuwaingiza David Polepole na Wylin Dalvin.

Hata hivyo, dakika ya 62 ndipo mambo yalipobadilika baada ya Sulwe kuamua Mombasa ipate penalti, akidai mchezaji wake alivutwa jezi ndani ya eneo la hatari.

Uamuzi huo uliibua hasira kwa wachezaji na mashabiki wa Sharks, hali iliyosababisha mechi kusimama na hatimaye kuachwa bila kuendelea.

Sasa macho yote yameelekezwa kwa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), ambalo linatarajiwa kuamua hatma ya mchezo huo na timu zitakazoshiriki Ligi Kuu msimu huu.

Kifungu cha 3.5.6 cha Kanuni na Taratibu za FKF kinasema: “Klabu itapoteza mchezo wowote uliositishwa kutokana na utovu wa nidhamu wa wanachama au mashabiki wake.”

Sharks ilimaliza nafasi ya tatu kutoka mwisho katika Ligi Kuu msimu uliopita, wakati Mombasa United ilimaliza nafasi ya tatu katika National Super League, hali iliyozifanya timu hizo kukutana katika mchujo wa kuwania nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu huu.