Banana Zoro: Picha za baba zinatuumiza
Muktasari:
- Akiwa mtoto wa nguli wa muziki wa dansi, Mzee Zahir Zorro, Banana amedumu katika sanaa kwa miaka mingi na kushuhudia mabadiliko makubwa ya muziki, kutoka enzi za redio na televisheni hadi zama za mitandao ya kijamii.
BANANA Zoro ni miongoni mwa wanamuziki wakongwe wenye mchango mkubwa katika muziki wa Bongo Fleva, akijenga jina kupitia nyimbo kama Mama yangu na Nipo Radhi, huku pia akionekana katika uigizaji katika tamthilia ya Huba.
Akiwa mtoto wa nguli wa muziki wa dansi, Mzee Zahir Zorro, Banana amedumu katika sanaa kwa miaka mingi na kushuhudia mabadiliko makubwa ya muziki, kutoka enzi za redio na televisheni hadi zama za mitandao ya kijamii.
Katika Dakika 5 za Mwanaspoti, Banana Zoro anazungumzia wasanii anaowakubali, kuimba ‘live’, siri ya kudumu kwenye muziki, ushauri kwa vijana, pamoja na hali ya baba yake na ombi la familia kwa wanaomtembelea.
MWANASPOTI: Kizazi kipya cha muziki unakionaje kwa upande wa ubora wa kazi?
BANANA ZORO: Kuna vijana wengi wanafanya vizuri na wana vipaji. Mimi napenda msanii anayejua anachokifanya na anayezingatia ubora wa kazi yake.
MWANASPOTI: Ni wasanii gani wa kizazi kipya unaowakubali zaidi?
BANANA ZORO: Nandy na Vanilla. Nawapenda kwa sababu wana uwezo mzuri wa kuwasilisha kazi zao na wanaweza kuimba moja kwa moja bila kutegemea ‘playback’.
MWANASPOTI: Kwa nini unaona kuimba ‘live’ ni muhimu kwa msanii?
BANANA ZORO: Ni muhimu sana kwa sababu ndipo unapoonyesha uwezo wako halisi. Msanii akiwa jukwaani anatakiwa aweze kuimba na kuwafanya watu wafurahie bila kutegemea sauti iliyorekodiwa.
MWANASPOTI: Umeweza kudumu kwenye muziki kwa miaka mingi. Siri yako ni nini?
BANANA ZORO: Ni nidhamu ya kazi, kuheshimu mikataba, kuwa mwaminifu kwa mashabiki na kuwa na mahusiano mazuri na wanamuziki ambao tunafanya nao kazi.
MWANASPOTI: Mitandao ya kijamii imebadilisha nini kwenye muziki wa sasa?
BANANA ZORO: Imebadilisha mambo mengi. Zamani msanii alitegemea zaidi redio na televisheni kuwafikia mashabiki, lakini sasa TikTok, Instagram na YouTube zinamwezesha kuwafikia mashabiki moja kwa moja.
MWANASPOTI: Ungependa kuwashauri nini wasanii wanaochipukia?
BANANA ZORO: Wazingatie matumizi ya lugha kwenye kazi zao. Muziki una uwezo wa kubaki kwa vizazi vingi, hivyo ni vizuri kutengeneza kazi zenye ujumbe mzuri na zinazoweza kusikilizwa na vizazi vijavyo.
MWANASPOTI: Mbali na muziki, tunakuona pia kwenye tamthilia ya Huba. Uigizaji umeingiaje kwenye maisha yako?
BANANA ZORO: Napenda sanaa kwa ujumla. Muziki ndio sehemu yangu kubwa, lakini uigizaji nao ni eneo ambalo nimekuwa nikijifunza na kulifurahia.
MWANASPOTI: Baba yako, Mzee Zahir Zorro, anaendeleaje kiafya?
BANANA ZORO: Kwa sasa anaendelea vizuri. Kikubwa zaidi ni uhai. Kuna wakati anakuwa siyo sawa, lakini kwa jumla yuko vizuri.
MWANASPOTI: Kumekuwa na watu wanaomtembelea na kupiga picha au video akiwa katika hali yake ya ugonjwa. Familia inalichukuliaje jambo hilo?
BANANA ZORO: Kwa kweli kauli ya Steve Nyerere ilikuja wakati sahihi kwa sababu iligusa kitu ambacho hata sisi familia tulikuwa tunakiona. Baba ni mtu mcheshi, mkarimu na anayependa kupiga picha na watu, lakini kwa sasa yuko kwenye hali ya ugonjwa. Picha na video zinazochukuliwa akiwa katika hali hiyo na kusambazwa mitandaoni hazitupendezi kama familia.
Tunaomba watu wanaokwenda kumjulia hali na kumfariji wazingatie staha na faragha yake katika kipindi hiki. Tunawashukuru wote wanaoendelea kumuombea na kumtembelea kwa nia njema.
MWANASPOTI: Kwa nini familia ililazimika kudhibiti matumizi ya simu ya Mzee Zorro?
BANANA ZORO: Baba ni mtu mkarimu anayependa kupokea simu na kuzungumza na kila anayempigia. Lakini kwa hali yake ya sasa, simu nyingi zilikuwa zikimchosha. Tunaomba wanaotaka kujua maendeleo yake wawasiliane na familia badala ya kumpigia moja kwa moja.
MWANASPOTI: Ukiangalia safari yako yote ya muziki, ni jambo gani unalojivunia zaidi?
BANANA ZORO: Najivunia nimeweza kufanya muziki kwa muda mrefu na bado nina nafasi ya kuendelea kufanya kazi, kusaidia vijana na kushirikiana na watu wengine katika sanaa.