Messi afunga ukurasa Argentina, aaga kwa bao, asisti mbili
Muktasari:
- Messi, mwenye umri wa miaka 39, alifunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao katika usiku uliojaa hisia mbele ya zaidi ya mashabiki 85,000.
Lionel Messi ameaga rasmi timu ya taifa ya Argentina kwa namna ya kipekee baada ya kuiongoza kushinda mabao 3-0 dhidi ya Benin katika mchezo wake wa mwisho wa kimataifa kwenye Uwanja wa Monumental.
Messi, mwenye umri wa miaka 39, alifunga bao moja na kutoa pasi mbili za mabao katika usiku uliojaa hisia mbele ya zaidi ya mashabiki 85,000.
Baada ya mchezo huo, Messi alishindwa kuzuia machozi huku akizungumza kuhusu miaka yake zaidi ya 20 akiwa na jezi ya Argentina.
"Ninapofikiria siku hii, jambo la kwanza ninalomfikiria ni baba yangu," amesema Messi, ambaye hivi karibuni amempoteza baba yake mzazi.
Messi ameondoka Argentina akiwa mchezaji mwenye mechi nyingi zaidi, akifikisha michezo 208 huku akiwa kinara wa mabao kwa kufunga 126. Pia ameiongoza Argentina kushinda Copa America, Kombe la Dunia na mataji mengine makubwa.
Nyota mbalimbali wa soka wa Argentina wamemzungumzia Messi kama mchezaji wa kipekee.
Rodrigo De Paul amemuelezea Messi kama mtu aliyekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo yake ndani na nje ya uwanja, akisisitiza namna alivyomsaidia kukua katika maisha ya soka.
Nicolás Otamendi, ambaye pia amecheza mechi yake ya mwisho kwa Argentina, amesema ni bahati kubwa kwake kuwa sehemu ya safari ya Messi na kushiriki naye katika nyakati muhimu za timu hiyo.
Emiliano Martínez naye amemshukuru Messi kwa kile alichowafanyia yeye na taifa la Argentina, akisema ni heshima kubwa kwake kuwa sehemu ya historia ya nahodha huyo.
Cristian Romero amesema anampenda na kumshukuru Messi kwa kila kitu alichomwachia yeye binafsi pamoja na Argentina.
Enzo Fernández ameeleza kuwa alipokuwa akiingia kwenye timu ya taifa alikuwa na ndoto ya kucheza pamoja na Messi, lakini alichokutana nacho kilikuwa zaidi ya kucheza na sanamu yake, kwani Messi alimkaribisha na kumsaidia kujisikia sehemu ya timu.
Leandro Paredes amesema Argentina itaendelea kumshukuru Messi kwa kila kitu alichowafanyia, akisisitiza kuwa alikuwa na bahati ya kushiriki naye safari hiyo.
Kocha Lionel Scaloni pia amesema ana deni la shukrani kwa Messi kwa kuwa sehemu ya safari yake ya Argentina, akiielezea historia yao kama safari ya kipekee iliyomalizika kwa mafanikio makubwa.
Usiku huo haukuwa tu wa kumuaga mchezaji, bali uliashiria mwisho wa enzi ya Messi katika timu ya taifa. Baada ya filimbi ya mwisho, wachezaji wenzake na wapinzani walimzunguka na kumkumbatia, huku mashabiki wakiimba jina lake.
Katika mchezo huo, Messi alitoa pasi ya bao la kwanza kwa Otamendi, akamsaidia Nico Paz kufunga la pili kabla ya yeye mwenyewe kufunga kwa penalti na kufikisha bao lake la 126 kwa Argentina.
Baada ya hapo, Uwanja wa Monumental uligeuka kuwa eneo la sherehe, huku kukiwa na maonyesho ya ndege zisizo na rubani angani na burudani maalumu ya kumuaga mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi katika historia ya Argentina.
Messi amefunga safari yake ya Argentina akiwa na Kombe la Dunia la 2022, mataji mawili ya Copa America na kumbukumbu ya kuwa mchezaji aliyeibeba timu hiyo katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili.
"Kuacha kuja hapa kutaniuma sana. Ningependa kuendelea kuja maisha yangu yote, kwa sababu kuichezea Argentina ni jambo zuri zaidi linaloweza kumpata mchezaji," amesema Messi katika ujumbe wake wa mwisho.