Federico Chiesa njia nyeupe kuondoka Liverpool
Muktasari:
- Chiesa kwa sasa yuko nje ya uwanja kutokana na jeraha la misuli, huku Liverpool ikitarajia kurejea kwake mazoezini wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa baadaye mwezi huu.
Mshambuliaji wa Italia, Federico Chiesa, 28, yuko tayari kuondoka Liverpool dirisha la usajili la Januari endapo atashindwa kupata nafasi ya kutosha ya kucheza baada ya kurejea kutoka kwenye jeraha.
Chiesa kwa sasa yuko nje ya uwanja kutokana na jeraha la misuli, huku Liverpool ikitarajia kurejea kwake mazoezini wakati wa mapumziko ya mechi za kimataifa baadaye mwezi huu.
Hata hivyo, hali yake imezidi kuwa ngumu baada ya kocha mpya Andoni Iraola kumuacha nje ya kikosi kitakachoshiriki Ligi ya Mabingwa msimu huu kwa mara ya pili mfululizo.
Chiesa alibaki Liverpool katika dirisha la usajili lililopita licha ya kuhusishwa na uwezekano wa kurejea Serie A, lakini sasa anaonekana kuwa tayari kutafuta changamoto mpya iwapo hatapata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Taarifa zinaeleza kuwa uamuzi wake wa kuondoka Januari utategemea kiwango cha muda wa kucheza atakachopewa baada ya kupona.
Chiesa alijiunga na Liverpool akitokea Juventus mwaka 2024, lakini amekuwa akipambana kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza kutokana na ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji na matatizo ya majeraha.
Jadon Sancho
WINGA wa zamani wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Jadon Sancho, mwenye umri wa miaka 26, anadaiwa kuwa kwenye mazungumzo na angalau klabu mbili za Ligi Kuu England kuhusu uwezekano wa kujiunga na moja kati ya hizo.
Serge Aurier
BEKI wa zamani wa Tottenham Hotspur, Serge Aurier, 33, yuko mbioni kufanya uamuzi wa kushangaza katika hatua za mwisho za maisha yake ya soka, akitarajiwa kujiunga na Montigny-en-Gohelle ya Daraja la Saba Ufaransa. Aurier aliisaidia Spurs kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2019, sasa ni mchezaji huru.
Matheus Mane
LIVERPOOL na Manchester United zimeanza mawasiliano ya moja kwa moja na Wolves kuhusu uwezekano wa kumsajili winga wa timu ya taifa ya Ureno chini ya miaka 21, Matheus Mane, mwenye umri wa miaka 18.
Renato Sanches
CHELSEA inadaiwa kumfikiria kiungo Renato Sanches, 29, kama chaguo la nafasi ya Enzo Fernandez, huku mchezaji huyo wa zamani wa Swansea akiwa tayari huru baada ya PSG kuvunja mkataba wake. Sanches amekuwa na kipindi kigumu katika miaka ya hivi karibuni, akitumia misimu minne PSG.
Julian Alvarez
MSHAMBULIAJI wa Atletico Madrid, Julian Alvarez (26), alinyimwa nafasi ya kutimiza ndoto yake ya kujiunga na Barcelona kabla ya dirisha la usajili kufungwa, huku akionekana bado kutoridhishwa na uamuzi huo. Atletico ilikataa kumuuza mshambuliaji huyo kwa wapinzani wao wa LaLiga kabla ya muda wa mwisho wa usajili.
Alex Baena
MANCHESTER City inafuatilia kwa karibu maendeleo ya kiungo wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Alex Baena, mwenye umri wa miaka 25, lakini inaelezwa kuwa huenda isifanye uamuzi wa kumsajili katika dirisha la Januari.
Endrick
AC Milan inajiandaa kumnasa mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil, Endrick, mwenye umri wa miaka 20, kwa mkopo kutoka Real Madrid katika dirisha la usajili la Januari, mwakani.