Duh! Barcelona yapata pigo, Yamal kukaa nje mwezi
Muktasari:
- Kikosi hicho cha kocha Hansi Flick kiliangusha pointi kwa mara ya tano katika mechi katika mechi za ligi baada ya mkali wa Leganes, Sergio Gonzalez kufunga bao pekee katika mechi hiyo iliyofanyika Jumapili iliyopita uwanjani Estadi Olimpic Lluis Companys.
BARCELONA, HISPANIA: BARCELONA imethibitisha winga wao Lamine Yamal atakuwa nje ya uwanja kwa wiki tatu hadi nne baada ya kupata maumivu ya enka kwenye mchezo wa kipigo kutoka kwa Leganes kwenye mikikimikiki ya La Liga, wikiendi iliyopita.
Kikosi hicho cha kocha Hansi Flick kiliangusha pointi kwa mara ya tano katika mechi katika mechi za ligi baada ya mkali wa Leganes, Sergio Gonzalez kufunga bao pekee katika mechi hiyo iliyofanyika Jumapili iliyopita uwanjani Estadi Olimpic Lluis Companys.
Barcelona pengine ilimaliza wikiendi ikiwa kwenye kilele cha msimamo wa La Liga, lakini matokeo hayo ya kichapo yamewafanya kufikiwa na Atletico Madrid wakilingana pointi, huku ikiizidi Real Madrid kwa pointi moja tu kwenye nafasi ya tatu.
Na bahati mbaya kwa Barcelona, wakati ikipata matokeo mabaya uwanjani mambo yamekuwa mabaya zaidi kwao baada ya winga wao matata Yamal kuumia enka.
Staa huyo wa kimataifa wa Hispania alipata maumivu hayo kipindi cha kwanza, lakini alicheza hadi kipindi cha pili dakika 75 alipotoka na kuingia Gavi.
Juzi Jumatatu, iliripotiwa Yamal, 17 angefanyiwa uchunguzi zaidi wa kufahamu ukubwa wa tatizo lake na hapo ndipo ilipogundulika atakuwa nje kwa mwezi mzima baada ya kupata tatizo kwenye enka ya mguu wake wa kulia.
Kukosekana kwa Yamal ni pigo kubwa kwa Barca kutokana na winga huyo kufunga mabao sita na kuasisti mara 12 katika mechi 21 alizocheza msimu huu.
Kutokana na hilo, staa huyo wa Barca hatakuwapo kwenye mechi ya vita ya kuongoza ligi dhidi ya Atletico Madrid, Jumamosi.
Yamal anaweza kukosa pia mechi za Spanish Super Cup, dhid ya Athletic Bilbao itakayopigwa Saudi Arabia, Januari 8 na dhidi ya Real Madrid au Mallorca kama itafika fainali, Januari 12.