DR Congo yacheza kwa siri kuhofia ebola
Muktasari:
- DR Congo inatarajiwa kucheza dhidi ya Chile katika Mji wa Orleans, Ufaransa, lakini tahadhari kali zimewekwa ili kuzuia hatari yoyote inayoweza kutokea.
ORLEANS, UFARANSA: Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) italazimika kucheza mechi yake ya mwisho ya maandalizi ya Kombe la Dunia bila mashabiki baada ya mamlaka kuamua mechi hiyo ifanyike milango ikiwa imefungwa kutokana na hofu ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola unaoendelea nchini humo.
DR Congo inatarajiwa kucheza dhidi ya Chile katika Mji wa Orleans, Ufaransa, lakini tahadhari kali zimewekwa ili kuzuia hatari yoyote inayoweza kutokea.
Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Cadiz, Hispania, lakini meya wa eneo hilo alisaini amri maalumu ya kuzuia mechi hiyo kufanyika kama hatua ya tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Taarifa zinaeleza Marekani, ambayo ni moja ya nchi mwenyeji wa Kombe la Dunia, imeweka masharti makali yanayowataka wachezaji na viongozi waliotoka DR Congo kukaa nje ya nchi hiyo kwa siku 21 bila kuonyesha dalili za ugonjwa huo kabla ya kuruhusiwa kuingia.
Hata hivyo, inaelezwa hakuna mchezaji wa DR Congo aliyeitembelea nchi yao hivi karibuni kwa kuwa wote wanacheza soka katika klabu za nje ya nchi.
Baadhi ya mashabiki na viongozi wa timu ndio wanaoripotiwa kusafiri kutoka DR Congo kwenda Ulaya.
Kikosi hicho kimekuwa kikifanya maandalizi yake Hispania baada ya kumaliza kambi ya siku 10 Ubelgiji na kilicheza mechi mbili dhidi ya Denmark zilizoisha kwa suluhu.
DR Congo imeandika historia baada ya kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1974 iliposhiriki mashindano hayo kwa jina la Zaire.
Katika ushiriki wao wa kwanza walimaliza mkiani mwa kundi lao baada ya kufungwa na Scotland, Brazil na Yugoslavia.
Safari hii matumaini ni makubwa zaidi huku wakipanga kuweka kambi yao Houston, Marekani wakati wa mashindano.
Watacheza mechi yao ya kwanza ya Kundi K dhidi ya Ureno Juni 17 kabla ya kukutana na Colombia na baadaye Uzbekistan.
Mlipuko wa sasa wa Ebola katika eneo la mashariki mwa DR Congo unasababishwa na aina adimu ya virusi inayojulikana kama Bundibugyo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema hadi sasa hakuna chanjo iliyothibitishwa kwa aina hiyo na inaweza kuchukua hadi miezi tisa kutengeneza chanjo mpya.
Kutokana na hali hiyo, maandalizi ya DR Congo Kombe la Dunia yanaendelea chini ya uangalizi mkubwa wa kiafya.