Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Siasa zamuondoa Paolo Maldini italia

MALDINI Pict
MALDINI Pict

Muktasari:

  • Pirlo, ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuinoa Azzurri kwa pendekezo la Maldini, ameshindwa kutwaa nafasi hiyo baada ya wanasiasa kadhaa wa Italia kupinga uhusiano wake wa kibiashara na kampuni ya kamari ya Urusi, Fonbet.

MILAN, ITALIA: SOKA la Italia limeingia kwenye sintofahamu baada ya vigogo Paolo Maldini na Leonardo kujiuzulu nyadhifa zao kufuatia sakata la Andrea Pirlo kuondolewa kwenye mbio za kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo.

Pirlo, ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuinoa Azzurri kwa pendekezo la Maldini, ameshindwa kutwaa nafasi hiyo baada ya wanasiasa kadhaa wa Italia kupinga uhusiano wake wa kibiashara na kampuni ya kamari ya Urusi, Fonbet.

Awali, Pirlo alikuwa karibu kufikia makubaliano ya kuinoa Italia, hasa baada ya taarifa kudai kuwa makocha nyota Pep Guardiola na Carlo Ancelotti walikataa ofa ya kuifundisha timu hiyo.

Hata hivyo, mpango huo ulivurugika baada ya kuibuka kwa mjadala kuhusu nafasi ya Pirlo kama balozi wa Fonbet, jambo lililoibua maswali kutokana na msimamo wa Italia kuhusu vita kati ya Urusi na Ukraine.

Katika msukosuko huo, Maldini anaripotiwa kukasirishwa na uamuzi wa Rais wa Shirikisho la Soka la Italia (FIGC), Giovanni Malago, wa kuzuia uteuzi wa Pirlo na kuamua kuachia wadhifa wake wa Mkurugenzi wa Ufundi akiwa ametumikia siku 16 pekee. Msaidizi wake, Leonardo, naye ameondoka sambamba naye.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Pirlo alithibitisha kuwa hayupo tena kwenye mchakato wa kupewa kazi hiyo, akisisitiza kuwa ushirikiano wake na Fonbet ulitokana na kazi yake ya ukocha katika klabu ya Dubai United, huku ukilenga masuala ya kibiashara na michezo pekee.

"Nimefuatilia kwa masikitiko makubwa mjadala ulioibuka kuhusu jina langu na uwezekano wa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Italia. Kwa heshima kwa taasisi na shirikisho, nilichagua kukaa kimya hadi sasa," amesema Pirlo.

Ameongeza kuwa katika maisha yake yote ya soka amekuwa akifanya kazi kwa kuzingatia sheria za nchi alizofanya kazi na mikataba aliyosaini, akisisitiza kuwa ushirikiano wake na Fonbet haukuwa na malengo ya kisiasa.

Hata hivyo, kauli hiyo imepingwa na mmiliki wa Dubai United, Sergey Lomakin, aliyedai kuwa ushirikiano wa Pirlo na kampuni hiyo haukuwa sehemu ya lazima ya mkataba wake na klabu hiyo.

Pirlo pia aliwashukuru Maldini na Leonardo kwa imani waliyoonyesha kwake, akieleza kusikitishwa na jinsi suala la kiufundi lilivyogeuzwa mjadala wa kisiasa.

"Ninaipenda Italia bila kujali nafasi yoyote ya kazi. Hilo ni sehemu ya historia na utambulisho wangu," amesema.

Italia sasa imelazimika kuanza upya mchakato wa kutafuta kocha mpya. Baada ya Ancelotti, Guardiola na sasa Pirlo kuondoka kwenye mbio hizo, majina ya makocha wa zamani wa Azzurri, Roberto Mancini na Antonio Conte, yamerudi kupewa nafasi ya kuiongoza timu hiyo ambayo imeshindwa kufuzu Kombe la Dunia mara tatu mfululizo.