Declan Rice ‘kulamba’ mkataba Arsenal
Muktasari:
- Rice, 27, amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Arsenal tangu alipohamia kutoka West Ham United kwa ada ya pauni105 milioni Julai 2023.
LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa Arsenal, Declan Rice, yuko katika hatua za mwisho za kukubaliana mkataba mpya wa muda mrefu na klabu hiyo, kwa mujibu wa taarifa za BBC Sport.
Rice, 27, amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Arsenal tangu alipohamia kutoka West Ham United kwa ada ya pauni105 milioni Julai 2023.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao, lakini mazungumzo ya kuongeza mkataba yamekuwa yakiendelea na sasa yamefikia hatua nzuri.
Taarifa zinaeleza kuwa Rice atapewa ongezeko kubwa la mshahara wake unaoripotiwa kuwa pauni 240,000 kwa wiki, hatua itakayomfanya alingane na anayelipwa zaidi klabuni hapo, Bukayo Saka, anayekadiriwa kuvuna karibu pauni 350,000 kwa wiki.
Tangu alipowasili Arsenal, Rice amecheza mechi 165 na alikuwa sehemu muhimu ya kikosi kilichosaidia klabu hiyo kuvunja ukame wa miaka 22 bila kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu uliopita.
Kwa upande wa timu ya taifa England, Rice ana jumla ya mechi 80 tangu abadilishe uamuzi wa kuichezea England baada ya awali kuichezea Jamhuri ya Ireland.
Ingawa alijiondoa kwenye kikosi cha England kilichoitwa na kocha Thomas Tuchel kabla ya kambi ya hivi karibuni ya wiki tatu, kiungo huyo bado anaendelea kuwa sehemu muhimu ya mipango ya kocha huyo.
Tuchel amewahi kumsifu Rice akimtaja kuwa miongoni mwa “viungo bora zaidi barani Ulaya”.
Rice anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Arsenal kitakachowakaribisha Leeds United katika mchezo wa Ligi Kuu England kesho Jumamosi.
Hatua hiyo ya Rice kuongeza mkataba inakuja siku chache baada ya Arsenal kumtangaza kocha Mikel Arteta kusaini mkataba mpya wa miaka minne hadi mwaka 2030, huku akitajwa kuwa kocha anayelipwa zaidi katika Ligi Kuu England.
Arteta, ambaye alikabidhiwa mikoba ya Arsenal Desemba 2019, amefungiwa mkataba mpya utakaomfanya aendelee kukaa Emirates hadi 2030.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, kocha huyo mwenye umri wa miaka 44 atalipwa mshahara wa pauni17 milioni (zaidi ya Sh40 bilioni) kwa mwaka, huku akiwa na nafasi ya kuongeza hadi pauni milioni tatu kupitia bonasi.