Kane awabwaga tena Ronaldo, Messi
Muktasari:
- Kane alifunga bao la pili katika ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Club Brugge kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufanikiwa kuifikia rekodi hiyo tamu.
MUNICH, UJERUMANI: STRAIKA wa Bayern Munich, Harry Kane ameweka rekodi mpya usiku wa Jumatano baada ya kufunga bao lake la 20 la msimu akiwa amecheza mechi 12 pekee jambo ambalo hata Cristino Ronaldo na Lionel Messi hawakuwahi kulifanya.
Kane alifunga bao la pili katika ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Club Brugge kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufanikiwa kuifikia rekodi hiyo tamu.
Kwa mujibu wa kampuni ya takwimu za michezo Opta, bao la dakika ya 14 dhidi ya Brugge lilimfanya Kane kufikisha mabao 20 msimu huu na kuwapita Messi na Ronaldo.
Ronaldo pekee ndiye anayeikaribia kidogo rekodi hii kwani aliwahi kufunga mabao 20 katika mechi 13 msimu wa 2014-15, huku Messi akiwahi kufikisha mabao 20 katika mechi 17 mara kadhaa.
Takwimu hizi zinaonyesha huenda Kane akaweka rekodi nyingi zaidi kwa msimu huu jambo litakalomfanya kuwa na nafasi kubwa ya kushinda tuzo kubwa kama ya Ballon D'or.
Akizungumzia kiwango chake, kocha wa Bayern Vincent Kompany alimpongeza Kane kwa mwanzo mzuri na kumlinganisha na Messi na Ronaldo.
"Harry Kane bado anaweza kufanya zaidi ya hiki lakini hafi kufikia sasa amekuwa mchezaji wakipekee sana kwetu. Nafikiri Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wamepata mafanikio makubwa kiasi cha kwamba kile kinachofanywa na Kane kwa sasa kinaonekana kuwa cha kawaida, lakini niseme tu, Kane anafanya kitu cha ajabu sana. Siwezi kumfundisha Kane jinsi ya kupiga mipira ya kichwa kwa ustadi kama anavyofanya. Kuna mambo mengine huwezi kufundisha ni kipaji halisi."