De Bruyne amjibu mtu hovyo
Muktasari:
- Ubelgiji ilisukumwa nje kwenye fainali hizo za Ujerumani katika hatua hiyo ya 16 bora baada ya kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Ufaransa, ambapo beki Jan Vertonghen alijifunga kwenye dakika za mwishoni.
DORTMUND, UJERUMANI: STAA, Kevin De Bruyne amembwatukia mwandishi wa habari na kusikika akisema “mpumbavu” baada ya kuulizwa swali la kijinga kufuatia Ubelgiji kutupwa nje ya fainali za Euro 2024 katika hatua ya mtoano ya 16 bora.
Ubelgiji ilisukumwa nje kwenye fainali hizo za Ujerumani katika hatua hiyo ya 16 bora baada ya kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Ufaransa, ambapo beki Jan Vertonghen alijifunga kwenye dakika za mwishoni.
Matokeo hayo yanafanya Ubelgiji iendelee kusubiri kunyakua taji la michuano mingine kwa miaka mingine zaidi na hapo ndipo mwandishi hiyo alipokuja na swali kwa De Bruyne alipomuuliza: “Ni ngumu kwa kiasi gani kwa ‘Kizazi cha Dhahabu’ kushindwa kufika fainali?”
De Bruyne, ambaye ni nahodha wa Ubelgiji alijaribu kulikataa swali hilo, alipoamua kuzitaja nchi nyingine ambazo pia zimesheheni mastaa kibao wenye vipaji vikubwa, alipojibu: “Nini, Kizazi cha Dhahabu?”
Hapo, ndipo ripota huyo aliposema, ‘Cha kwenu’, De Bruyne akajibu: “Cha kwenu?
“Na unasema Ufaransa na England na Hispania na Ujerumani hazina Vizazi vya Dhahabu?? Sawa, asante.”
Hayo ndiyo yalikuwa majibu ya De Bruyne na kuondoka kwenye chumba hicho cha waandishi wa habari, huku akisikika akisema ‘mpumbavu,’ na kutikisa kichwa akiwa haamini kilichotokea. Katika muongo uliopita, Ubelgiji iliibuka na kuwa moja ya mataifa makubwa kabisa katika soka la dunia.
Timu hiyo iliwahi kushika Namba Moja kwenye chati za FIFA kuanzia Novemba 2015 hadi Machi 2016 na ilirudi tena kwenye kilele kuanzia Septemba 2018 hadi Machi 2022. Lakini, kwa sasa, michuano mikubwa miwili mfululizo, imeshindwa kufika robo fainali.
Katika fainali za Kombe la Dunia 2022 huko Qatar, Ubelgiji ilishindwa kuvuka kwenye hatua ya makundi. Na huko nyuma ilitolewa na Italia kwenye robo fainali katika Euro 2020, ambako ilikuwa ikipewa nafasi kubwa baada ya kumaliza namba tatu kwenye Kombe la Dunia 2018.
Ubelgiji ilifika kwenye nane bora katika fainali za Euro 2016 na Kombe la Dunia 2014.