Daniel Dubois atwaa ubingwa wa WBO, wapinzani watano wakitajwa
Muktasari:
- Katika pambano hilo lililogeuka kuwa la kusisimua na la kukatisha tamaa, Dubois (28) alifanikiwa kunyanyuka baada ya kuangushwa chini mara mbili na kufanya mapinduzi makubwa yaliyompelekea kumaliza pambano kwa kumpiga Wardley kikatili kwenye raundi ya 11.
BONDIA Daniel Dubois amerejea kwa kishindo kwenye ramani ya ngumi za uzani wa juu duniani kufuatia ushindi mkubwa dhidi ya Fabio Wardley usiku wa kuamkia leo, pambano lililofanyika Co-op Live Arena, jijini Manchester, England.
Katika pambano hilo lililogeuka kuwa la kusisimua na la kukatisha tamaa, Dubois (28) alifanikiwa kunyanyuka baada ya kuangushwa chini mara mbili na kufanya mapinduzi makubwa yaliyompelekea kumaliza pambano kwa kumpiga Wardley kikatili kwenye raundi ya 11.
Ushindi huo umempa Dubois taji la uzani wa juu la WBO na kumfanya kuwa bingwa wa dunia mara mbili.
Kufuatia ushindi huo uliomvua Wardley hadhi ya kutoshindwa, wachambuzi wa masuala ya ngumi wameanza kuangalia wapinzani watano wanaoweza kuzichapa na Dubois katika pambano linalofuata.
Moses Itauma
Bondia huyu mwenye umri wa miaka 21 alikuwepo ukumbini akishuhudia pambano hilo, ikiwa ni miezi miwili tangu alipomchapa Jermaine Franklin katika ukumbi huo huo.
Mashabiki wengi nchini England wanatamani kushuhudia pambano hili ili kuona kama Itauma anaweza kuwa bingwa wa dunia mwenye umri mdogo zaidi katika historia ya nchi hiyo.
Oleksandr Usyk
Dubois ana hamu kubwa ya kulipiza kisasi cha vipigo viwili alivyopewa na Usyk.
Ingawa mashabiki hawana shauku kubwa ya kuona pambano la tatu, Usyk mwenyewe alikiri hivi karibuni kuwa Dubois yumo kwenye orodha ya mabondia watatu anaotaka kuzichapa nao kabla ya kustaafu.
Mshindi kati ya Tyson Fury vs Anthony Joshua
Pambano kubwa la kihistoria nchini England kati ya Fury na Joshua limeshasainiwa na linatarajiwa kupigwa Novemba mwaka huu, ilimradi tu AJ ashinde pambano lake la kujipima nguvu mwezi Julai.
Mshindi wa pambano hilo anaweza kuwa mpinzani mkuu wa Dubois hapo baadaye, ingawa Dubois hatasubiri pembeni kwa muda mrefu.
Deontay Wilder
Bingwa huyu wa zamani wa WBC alirudi kwenye chati mwezi uliopita baada ya kumstaafisha Derek Chisora. Wilder ana nia ya kuwa bingwa wa dunia kwa mara ya pili, na anaweza kuwa mpinzani sahihi kwa Dubois ambaye atapewa nafasi kubwa ya kushinda pambano hilo.
Pambano la Marudiano na Fabio Wardley
Mikataba ya mabondia hawa ilikuwa na kipengele cha pambano la marudiano, hivyo mashabiki wanaweza kushuhudia mechi nyingine kali.
Hata hivyo, pambano hilo halitarajiwi hivi karibuni kwani Wardley alipokea kipigo kizito na anahitaji mapumziko marefu hadi mwanzoni mwa mwaka ujao.