Curry alivyoizima Orlando akitupia pointi 56
Muktasari:
- Curry amefunga pointi 56 katika ushindi wa Golden State wa 121-115 dhidi ya Orlando na kutupia mitupio mitatu mara 12, ikiwa ni pamoja na mmoja kutoka mbali ya uwanja ambayo ilimaliza nusu ya kwanza akiwa kinara.
FLORIDA, MAREKANI: WAKATI Stephen Curry anapokuwa kwenye ubora wake kama ilivyokuwa huko Marekani kwenye hekaheka za michezo ya Ligi ya Kikapu (NBA), kocha wake Steve Kerr anajua tu kwamba lazima mwamba atatupia sana.
Curry amefunga pointi 56 katika ushindi wa Golden State wa 121-115 dhidi ya Orlando na kutupia mitupio mitatu mara 12, ikiwa ni pamoja na mmoja kutoka mbali ya uwanja ambayo ilimaliza nusu ya kwanza akiwa kinara.
Alionyesha tena umahiri wake katika uwanja wa mpira wa kikapu kuwa ni mchezaji anayekubalika kwa ubora zaidi katika kutupia mitupio mitatu.
“Amekuwa na pointi kama hizi kwa miaka miwili iliyopita. Alipofanya hivyo nilijua tu atafanya vizuri,” alisema kocha wa Warriors, Steve Kerr.
“Nilijihisi hivyo na nilidhani kuwa hiyo ilitengeneza jambo muhimu kwake.” Huo ni uthibitisho wa imani kubwa aliyonayo Kerr katika uwezo wa Curry. Hata wakati ambapo mambo hayaonekani kuwa mazuri, Curry ameweza kuwaokoa na kuleta mabadiliko makubwa kwenye mchezo.
Curry alirudi tena na kufunga pointi 22 dhidi ya Orlando katika robo ya tatu ya mechi yake ya 1,000 ya michuano ya msimu wa kawaida (regular season), akionyesha jinsi gani anavyoweza kubadilisha mchezo kipindi kifupi.
Huo ulikuwa ni ushahidi mwingine wa ubora wa Curry ambaye anaendelea kuthibitisha kuwa ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi katika historia ya NBA.
Hata hivyo, Curry alisema ushindi ulitokana na ushirikiano wa kitimu akisisitiza," wachezaji wengi walichangia katika ushindi, lakini ni vizuri kuwa na mfululizo kama huu na kufurahia.
Aliongeza kuwa ingawa alifurahi na kumaliza mchezo kwa kiwango cha juu alitambua mchango wa wachezaji wenzake, kusaidiana kufikia mafanikio.
Hiyo ilikuwa ni mechi ya 14 kwa Curry kufunga pointi 50 au zaidi akimpita Patrick Ewing na kupanda hadi nafasi ya 26 katika orodha ya wapachikaji wa pointi wa muda wote wa NBA kwa kuwa na pointi 24,867.
Pia alienda hadi nafasi ya 12 dhidi ya mastaa 19 katia utupiaji wa mitupio mitatu, akifunga zaidi ya 10 kwa mara ya 26 katika rekodi ya NBA.
Hata hivyo, pointi 56 alizozifunga zilikuwa ni sita nyuma ya rekodi yake ya maisha akiwa na kumbukumbu ya kufanya hivyo mara nyingi zaidi kuliko mchezaji yeyote mwingine wa NBA.
“Kwenye nusu ya kwanza tulikuwa na shida, lakini yeye alitufanya tuendelee kung'ara. Na aliendelea na hilo katika robo ya tatu akiuchukua kabisa mchezo,” alisema staa mwenzake, Draymond Green.
Hiyo ni ishara ya nguvu za kiakili za Curry ambaye anaweza kubadilisha mwelekeo wa mchezo kwa sekunde chache na kuwafanya wachezaji wenzake kuwa na imani zaidi.
Curry alikosa kwa pointi moja rekodi yake ya maisha katika pointi za mitupio mitatu, kwani aliwahi kufunga pointi 54 kwa mitupio mitatu 11 dhidi ya New York Knicks 2013 na 46 dhidi ya Oklahoma City Thunder 2016 akiwa na mitupio mitatu 12 ikionyesha kwa mara nyingine tena kuwa alizaliwa kwa ajili ya kufanya maajabu katika kikapu.
“Unapokuwa na usiku kama huu unapata pointi kwa njia mbalimbali, kwa sababu uko katika ubora na mpira unakufikia kwa wakati mzuri,” alisema Curry.
“Lakini inabidi kuwa na hatua nzuri, usawa na imani ya kutupia hata kama mpira unakuja kwa njia yoyote na kuwa tayari kwa wakati wako. Nimekuwa nikijaribu kila aina kushuti wakati fulani ili kuruhusu ubunifu wangu kutupa matokeo.”
WASIFU WAKE
Jina: Stephen Curry
Kuzaliwa: Machi 14, 1988 (umri 36)
Mahali: Akron, Ohio, Marekane
Urefu: futi 6 inchi 2
Jezi: 30:
Timu: Golden State Warriors
Nafasi: Point guard
Uzito: Kilo 84
Ligi: NBA