Kocha Senegal aapa kusahihisha makosa
Muktasari:
- Senegal ilianza kampeni yake kwa kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Algeria, matokeo yanayowaweka kwenye presha ya kutafuta ushindi katika mechi yake ya pili ili kubaki na matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali.
KOCHA wa timu ya taifa ya wanawake ya Senegal, Mame Moussa Cisse, amesema baada ya kupoteza mechi ya kwanza ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake dhidi ya Algeria kikosi hicho hakitaki kurudia makosa kwenye mechi ijayo dhidi ya Kenya.
Senegal ilianza kampeni yake kwa kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Algeria, matokeo yanayowaweka kwenye presha ya kutafuta ushindi katika mechi yake ya pili ili kubaki na matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali.
Akizungumzia hilo Cisse amesema timu hiyo iliwapa wapinzani nafasi nyingi za kucheza na kufanya makosa binafsi yaliyoigharimu timu, akisisitiza kuwa benchi la ufundi limeyafanyia kazi mapungufu hayo kabla ya kuivaa Kenya Julai 30.
“Tuliwaacha wapinzani wetu wapate nafasi nyingi na hii inatokana na makosa ya wachezaji wetu. Tumeyachambua na kujipanga kwa mchezo unaofuata dhidi ya Kenya,” amesema kocha huyo.
Senegal ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi A, ikihitaji ushindi dhidi ya Kenya ili kufufua matumaini ya kusonga mbele. Kenya nayo inaingia kwenye mchezo huo ikiwa imetoka kupokea kipigo cha mabao 4-0 dhidi ya wenyeji Morocco.
Morocco inaongoza kundi hilo baada ya kuanza vizuri ikichapa Kenya, huku Algeria ikishika nafasi ya pili kufuatia ushindi dhidi ya Senegal. Hali hiyo inafanya pambano kati ya Senegal na Kenya kuwa la kuamua hatima ya timu hizo mbili kwenye mbio za kufuzu hatua ya mtoano.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, kwani timu zote mbili zinahitaji pointi tatu ili kusaka nafasi ya robo fainali.