Cristiano Ronaldo bado 19
Muktasari:
- Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, aliifungia bao la pili Al Nassr katika dakika ya 42, baada ya kupokea mpira uliotengenezwa kwa ushirikiano wa Sadio Mané na Aiman Yahya, kabla ya mshambuliaji huyo kupiga shuti lililojaa wavuni.
RIYADH, SAUDI ARABIA: NYOTA wa Ureno, Cristiano Ronaldo, ameendelea kuandika historia katika soka, baada ya kufunga bao lake la 981, akiisaidia Al Nassr kuichapa Neftchi Fergana ya Uzbekistan mabao 3-1 katika Ligi ya Mabingwa Asia, juzi Oktoba 12, 2026.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, aliifungia bao la pili Al Nassr katika dakika ya 42, baada ya kupokea mpira uliotengenezwa kwa ushirikiano wa Sadio Mané na Aiman Yahya, kabla ya mshambuliaji huyo kupiga shuti lililojaa wavuni.
Bao hilo limemfanya Ronaldo kubakiwa na mabao 19 kufikisha 1,000, hatua ambayo itakuwa rekodi kubwa kwa mshambuliaji huyo anayeendelea kucheza katika kiwango cha juu akiwa na Al Nassr na timu ya taifa ya Ureno.
Kwa mujibu wa takwimu, wachezaji wanne ndio wamefikia rekodi ya mabao 1,000 katika hesabu inayojumuisha mechi rasmi na baadhi ya mechi za kirafiki.
Miongoni mwao ni gwiji wa Brazil, Pelé, ambaye ameorodheshwa kuwa na mabao 1,274, Josef Bican wa Austria na Czechslovakia akiwa na mabao 1,081, Ronaldo akiwa na mabao 1,025 na Ferenc Puskás wa Hungary akiwa na mabao 1,011.
Takwimu hizo hazimaanishi kuwa wote wamefunga mabao hayo katika mechi rasmi pekee. Katika orodha ya mabao ya mechi rasmi, Ronaldo ana mabao 978, Pelé 770, Bican 743 na Puskás 760.
Kwa hiyo, Ronaldo anaendelea kuikaribia rekodi ya kufikisha mabao 1,000 katika hesabu ya mechi rasmi, huku jina la Pelé likibaki kuwa sehemu muhimu ya mjadala kuhusu wafungaji bora wa historia ya soka.
Ushindi wa Al Nassr umekuja katika mchezo ulioanza kwa kuchelewa kwa takribani saa moja kutokana na tahadhari ya usalama iliyotolewa Riyadh, kufuatia tishio la mashambulizi ya makombora yaliyohusishwa na waasi wa Kihouthi kutoka Yemen.
Tahadhari hiyo ilitolewa dakika 15 kabla ya muda uliopangwa wa kuanza mchezo.
Baada ya hali ya usalama kutathminiwa, pambano hilo liliruhusiwa kuchezwa katika Uwanja wa Al-Awwal Park.
Al Nassr ilianza kupata bao la Angelo dakika ya 33, kabla ya Ronaldo kuongeza la pili dakika tisa baadaye.
Neftchi Fergana ilipunguza pengo kupitia Alisher Odilov dakika ya 51, lakini kadi nyekundu kwa Ikromjon Alibaev dakika ya 65 na bao la kujifunga la Anvarjon Gofurov dakika ya 78 viliipa Al Nassr ushindi wa mabao 3-1.