Coventry City wafunga bao daaba ya miaka 25
Muktasari:
- Ushindi huo wa kishindo umeipa timu hiyo inayofundishwa na Frank Lampard nguvu mpya, huku ikionyesha haiwezi tena kuchukuliwa kama timu ya kuchezea katika ligi hiyo yenye ushindani mkubwa.
COVENTRY, ENGLAND: MASHABIKI wa Coventry City wameandika ukurasa mpya wa historia baada ya timu yao kuichapa Newcastle United mabao 4-1 katika mchezo wa Ligi Kuu England, usiku wa kipekee uliowashuhudia wakishangilia mabao manne ya nyumbani baada ya kusubiri kwa siku 9,310.
Ushindi huo wa kishindo umeipa timu hiyo inayofundishwa na Frank Lampard nguvu mpya, huku ikionyesha haiwezi tena kuchukuliwa kama timu ya kuchezea katika ligi hiyo yenye ushindani mkubwa.
Jack Rudoni, Sidiki Cherif, Ellis Simms na Stephen Mfuni ndio waliotikisa nyavu za Newcastle katika mchezo ambao Coventry ilionyesha ubora mkubwa, hasa kipindi cha pili.
Bao la kwanza lilifungwa na Rudoni kwa mkwaju wa penalti dakika ya sita, kabla ya Cherif kuongeza la pili dakika tatu tu baada ya kuanza kwa kipindi cha pili. Simms na Mfuni wakafunga mabao mengine yaliyohitimisha usiku wa furaha kwa mashabiki wa Coventry.
RUDONI AANDIKA HISTORIA
Bao la Rudoni lilikuwa la kihistoria kwa Coventry, ambayo ilikuwa imesubiri kwa miaka 25 kushuhudia timu hiyo ikifunga bao la nyumbani katika Premier League.
Mara ya mwisho Coventry kufunga bao la ligi hiyo ikiwa nyumbani ilikuwa Aprili 16, 2001, katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Sunderland. Bao hilo lilifungwa na John Hartson katika uwanja wa zamani wa Highfield Road, ambao baadaye ulibomolewa.
Rudoni, ambaye alikuwa bado hajazaliwa wakati Hartson akifunga bao hilo, aliandika historia mpya kwa kufunga penalti iliyokuwa bao la kwanza la Coventry nyumbani katika Premier League kwenye uwanja wa Coventry Building Society Arena.
Penalti hiyo ilitokana na kipa wa Newcastle, Lukas Hornicek, kushindwa kudhibiti mpira uliokuwa ukiingia eneo la hatari kabla ya kumuangusha Cherif, aliyekuwa akijaribu kujiepusha na kugongana naye.
Mwamuzi John Brooks hakusita kuashiria penalti, huku teknolojia ya VAR ikiunga mkono uamuzi huo baada ya kubaini kulikuwa na mgusano mkubwa.