Dakika 90 za kazi Twiga Stars
Muktasari:
Twiga Stars inaingia katika mchezo huo wa marudiano ikihitaji matokeo ya sare ya aina yoyote ile ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele.
WAKIWA na mtaji wa bao 1-0 mfukoni, leo Oktoba 13 Timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga Stars’ inashuka kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam kukamilisha hesabu dhidi ya Botswana na kutinga hatua ya tatu ya mchujo wa kusaka tiketi ya Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles 2028.
Twiga Stars inaingia katika mchezo huo wa marudiano ikihitaji matokeo ya sare ya aina yoyote ile ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Gaborone, Twiga Stars ikiwa ugenini ilipata ushindi huo kupitia bao lililofungwa na nahodha wa timu hiyo, Opah Clement dakika ya 64, bao lililopunguza presha kwa Tanzania kwenye harakati za kutafuta mafanikio kwenye michuano.
Tanzania ambayo tayari ina mtaji wa bao moja inaingia kwenye mechi hiyo kumaliza kazi huku safu ya ushambuliaji ya timu hiyo inaoongozwa na Opah na wenzake Aisha Mnunka , Mary Siyame, Hasnath Ubamba anayekipiga Madrid FF ya Hispania ikitarajiwa kufanya makubwa kwenye mechi hiyo ya marudiano.
Wageni Botswana wanatarajiwa kuingia uwanjani kwa presha kubwa wakisaka bao la mapema ili kufuta faida ya Twiga Stars, hali inayotoa mwanya kwa wenyeji kutumia mbinu za kushambulia kwa kushtukiza kumaliza kazi mapema. Kama Twiga Stars itaiondoa Botswana na kutinga hatua ya tatu itakutana na mshindi kati ya Ethiopia na Rwanda. Kwenye mechi ya kwanza Ethiopia ikiwa ugenini imeshinda baon 1-0 dhidi ya Rwanda.
Mbali na mechi hiyo zitapigwa mechi nyingine 11 za michuano hiyo mapema saa 7:00 mchana Zimbabwe itakuwa nyumbani Harare kuvaana na Malawi, Equatorial Guinea ikiikaribisha Burkina Faso (saa 8:00 mchana), Nigeria ikiumana na Comoros (saa 9:00 alasiri), huku majira ya saa 10:00 jioni miamba mingine ikishuka dimbani Ethiopia ikicheza na Rwanda, Afrika Kusini ikivaana na Madagascar, na Ghana ikimenyana na Mauritius.
Shughuli hiyo itaendelea saa 11:00 jioni kwa Senegal dhidi ya Tunisia, Mali na Benin, pamoja na Algeria dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kabla ya Zambia kuialika Uganda saa 12:00 jioni pale Ndola na burudani hiyo kufungwa saa 1:00 usiku jijini Abidjan kwa pambano kali kati ya Ivory Coast na DR Congo.
Nahodha msaidizi wa Twiga Stars, Anastazia Katunzi amesema “tuna faida ya bao moja ugenini lakini mechi haijaisha tunawaomba mashabiki watusapoti na tupo tayari kupambana nyumbani ili tukamilishe kazi.”