Conte ajipigia chapuo Man United
Muktasari:
- Conte, 57, kwa sasa hana kazi baada ya kuachana na Napoli mwishoni mwa msimu uliopita, lakini kauli yake kuhusu aina ya klabu anayolenga imeongeza mjadala kuhusu uwezekano wa kurejea Ligi Kuu England.
MANCHESTER, ENGLAND: KOCHA Antono Conte ameibua hisia kuwa huenda akawa kwenye rada ya Manchester United baada ya kutoa kauli inayotafsiriwa kama dokezo la kutaka kuiongoza klabu hiyo iwapo Michael Carrick ataondoka Old Trafford.
Conte, 57, kwa sasa hana kazi baada ya kuachana na Napoli mwishoni mwa msimu uliopita, lakini kauli yake kuhusu aina ya klabu anayolenga imeongeza mjadala kuhusu uwezekano wa kurejea Ligi Kuu England.
Akizungumza na The Athletic, Conte alisema anatamani kujiunga na klabu yenye historia kubwa, lakini ambayo imepoteza mwelekeo wa kushindania mataji, akisisitiza kuwa angependa kuirudisha kwenye hadhi yake.
“Ukienda kwenye klabu ambayo historia yake inajieleza yenyewe, historia ya mataji, ubingwa wa ligi na ushindi,unaweza kuiheshimu historia hiyo kwa njia moja tu, kuwa na dhamira ya kuirudisha klabu kwenye malengo hayo,” alisema Conte.
“Unatengeneza historia kwa kushinda. Ningependa kwenda kwenye moja ya klabu hizo, kuifufua historia yake na kuifanya ing’ae tena.”
Kauli hiyo imehusishwa moja kwa moja na United, klabu ambayo haijashinda Ligi Kuu England tangu mwaka 2013, wakati Sir Alex Ferguson alipostaafu.
Kwa sasa, Carrick anakabiliwa na mwanzo mgumu wa msimu huku United ikiwa nafasi ya 12 kwenye msimamo baada ya kupata ushindi mmoja pekee katika mechi tano.
Iwapo hali hiyo itaendelea na uongozi ukaamua kumfuta kazi Carrick, Conte anaweza kuwa mmoja wa makocha watakaotajwa kwenye orodha ya wanaoweza kuchukua nafasi yake.
Conte anajulikana kwa kutumia mfumo wa 3-4-3, jambo ambalo lingeweza kuleta mabadiliko makubwa katika kikosi cha United.
Kipa Senne Lammens anaweza kupoteza nafasi yake, huku Conte akimrudisha Vanja Milinkovic-Savic, ambaye aliwahi kuwa kwenye vitabu vya United mwaka 2014–15 kabla ya kuondoka na kujijengea jina Torino.
Milinkovic-Savic pia aliwahi kufanya kazi chini ya Conte Napoli msimu uliopita na baadaye kuwa kipa namba moja wa Serbia.
Katika mfumo wa mabeki watatu, Lisandro Martinez anaweza kuwa mmoja wa nguzo muhimu katika safu hiyo, akishirikiana na mmoja kati ya Harry Maguire, Matthijs de Ligt au Leny Yoro.
Hata hivyo, kwa sasa hakuna uthibitisho rasmi kwamba United imemlenga Conte au kwamba kocha huyo ameomba kazi Old Trafford.
Lakini kauli yake kuhusu kutaka kuifufua klabu kubwa iliyopoteza makali imeifanya Manchester United ionekane kuwa miongoni mwa timu zinazoweza kuendana na maelezo hayo.