Clippers yakubali yaishe, Raptors washusha chuma!
Muktasari:
- Toronto itaifuata Clippers Novemba 2, mwaka huu na kuikaribisha Clippers Januari 1, mwakani. Timu hizo pia zimepangwa kukutana Vancouver katika mchezo wa maandalizi ya msimu (preseason) Oktoba 10, mwaka huu.
TORONTO, CANADA: BIASHARA ya kumhamisha Kawhi Leonard kutoka Los Angeles Clippers kwenda Toronto Raptors sasa imekamilika rasmi baada ya kucheleweshwa kwa miezi kadhaa kutokana na uchunguzi wa Shirikisho la Kikapu Marekani (NBA), kuhusu Clippers, unaohusisha kukwepa kanuni za ukomo wa mishahara.
Timu hizo awali zilikubaliana kuhusu dili hilo Juni 30, mwaka huu, lakini lilisimamishwa wakati ligi hiyo ikifanya uchunguzi kuhusu madai kwamba Clippers walikiuka kanuni za ukomo wa mishahara wakati wakimsajili Leonard kama mchezaji huru.
Clippers na Raptors zilikubaliana tena kuhusu masharti ya awali ya dili hilo Jumatatu wiki hii, kabla ya kulifanya rasmi kwa kuwasiliana na ofisi ya ligi.
Vyanzo vilisema Leonard alikubali kuachana na bonasi yake ya uhamisho yenye thamani ya Dola 7.45 milioni ili kusaidia kufanikisha uhamisho wake kwenda Toronto. Bonasi hiyo ingeifanya Raptors ivuke kiwango cha kwanza cha ukomo wa mishahara. Baada ya dili hilo kukamilika, Toronto itakuwa Dola 2.3 milioni chini ikiwa na mikataba 13 iliyohakikiwa.
LA Clippers itampokea Brandon Ingram, Gradey Dick, machaguo mawili ya raundi ya kwanza yasiyo ya ulinzi, haki ya kubadilishana chaguo moja la raundi ya kwanza na machaguo mawili ya raundi ya pili katika dili hilo. Uhamisho huo sasa utashughulikiwa baada ya Clippers kutumia siku 13 zilizopita kukabiliana na hatua za kinidhamu za ligi na kukamilisha taratibu za ndani.
NBA ilitangaza mapema mwezi huu orodha ya adhabu kali dhidi ya Clippers, ikiwa ni pamoja na kupokonywa machaguo matano ya raundi ya kwanza ya siku zijazo, faini ya Dola 30 milioni na kusimamishwa kwa mwaka mmoja kwa mmiliki Steve Ballmer kutokana na kukiuka kanuni za kukwepa kanuni ya ukomo wa mishahara katika kesi iliyomhusisha Leonard.
Adhabu hizo zilitolewa baada ya uchunguzi uliodumu karibu mwaka mmoja dhidi ya klabu hiyo, ambao “ulibaini mwenendo wa utovu wa nidhamu na ukiukaji mkubwa wa kanuni mara kadhaa” uliofanywa na Clippers, ambayo tayari ilikuwa imewahi kukiuka kanuni za mishahara. Awali, Leonard aliiongoza Raptors kushinda ubingwa wa kwanza wa NBA katika historia ya klabu hiyo mwaka 2019, kabla ya kuondoka Toronto msimu uliofuata na kusaini mkataba na Clippers.
Toronto itaifuata Clippers Novemba 2, mwaka huu na kuikaribisha Clippers Januari 1, mwakani. Timu hizo pia zimepangwa kukutana Vancouver katika mchezo wa maandalizi ya msimu (preseason) Oktoba 10, mwaka huu.