Dabi yaipeleka Simba Afrika Kusini
Muktasari:
- Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally, amesema kambi hiyo itaanza baada ya wachezaji kumaliza mapumziko ya siku saba yaliyotolewa kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara.
SIMBA imeamua kuondoka nchini na kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya kuweka kambi maalumu ya siku 10 huku uongozi wa klabu hiyo ukilenga kuipa timu utulivu na mazingira bora ya kujiandaa na ratiba nzito ya mwezi Oktoba.
Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally, amesema kambi hiyo itaanza baada ya wachezaji kumaliza mapumziko ya siku saba yaliyotolewa kufuatia ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Azam FC katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara.
Kwa mujibu wa Ahmed, wachezaji watatakiwa kurejea Septemba 23, kabla ya safari ya Afrika Kusini Septemba 24 ambapo timu itakaa kwa siku 10.
"Tumemaliza raundi sita za ligi kuu ya NBC tukiwa na mafanikio ya asilimia 100, tukishinda michezo yetu yote sita na kuchukua alama 18," amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa baada ya mchezo dhidi ya Azam FC, timu imeingia kwenye mapumziko kutokana na kalenda ya FIFA, hivyo uongozi ukaona ni wakati sahihi kuwapa wachezaji muda wa kupumzika kabla ya kurejea kambini.
AFRIKA KUSINI BADALA YA BONGO
Ahmed amesema sababu kubwa ya Simba kuchagua Afrika Kusini ni kutafuta mazingira yatakayowafanya wachezaji kubaki kwenye mkusanyiko na kuipa timu nafasi ya kufanya maandalizi bila usumbufu.
Amesema kambi za ndani zinaweza kuifanya timu kutumia muda mwingi katika usafiri kutokana na kutokuwepo kwa huduma zote muhimu katika eneo moja.
"Ukisema ukaweke kambi sehemu fulani inakulazimu hoteli iko hapa, uwanja uko kule, gym iko kule, bwawa la kuogelea liko kule. Inawalazimu kuwa na masafa ya kila siku," amesema.
Kwa upande mwingine, Ahmed amesema kukaa kambini nchini kunaweza pia kuwapa wachezaji nafasi ya kushughulika na mambo ya kijamii ambayo yanaweza kuvuruga umakini wao wakati wa maandalizi.
Ametoa mfano wa dharura mbalimbali za kifamilia na kijamii ambazo zinaweza kumfanya mchezaji kuomba ruhusa kutoka kambini.
RUSHINE, MAEMA WAMETANGULIA
Katika safari hiyo, baadhi ya wachezaji wa Simba wenye asili ya Afrika Kusini tayari wameondoka nchini kuelekea kwao.
Ahmed amewataja Rushine na Neo Maema kuwa miongoni mwa wachezaji ambao tayari wameshatangulia Afrika Kusini.
Amesema kocha mkuu Steve Barker pamoja na sehemu kubwa ya benchi lake la ufundi, ambao ni raia wa Afrika Kusini nao tayari wameelekea nchini humo.
Hivyo, timu itakaposafiri Septemba 24, itawakuta baadhi ya wachezaji na benchi la ufundi nchini humo kabla ya kuanza rasmi maandalizi ya kambi.
KAMBI YA NYOTA TANO
Ahmed amesema Simba imeandaa mazingira ya kiwango cha juu kwa ajili ya kambi hiyo, akifichua kuwa timu itaweka kambi katika hoteli ya nyota tano yenye huduma mbalimbali zinazohitajika kwa maandalizi ya kisasa ya mpira.
Ametaja uwepo wa gym, bwawa la kuogelea, kituo cha kurejesha utimamu wa mwili 'rehabilitation' pamoja na viwanja vya mazoezi katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Ahmed, mazingira hayo yamechaguliwa ili kuwawezesha wachezaji kufanya mazoezi, kupata muda wa kurejea katika hali bora ya kimwili na kujiandaa bila usumbufu.
Uamuzi huo, amesema, umeungwa mkono na rais wa heshima wa Simba, Mohammed Dewji ambaye alitaka timu ipate eneo lenye utulivu zaidi badala ya kuendelea kufanya maandalizi ya kila siku katika mazingira ya kawaida ya Dar es Salaam.
OKTOBA YA MOTO
Simba inaingia kambini ikijua kuwa baada ya mapumziko hayo, kazi kubwa ipo mbele yake. Ahmed amesema mwezi Oktoba utakuwa na ratiba yenye presha ikiwemo dabi ya Kariakoo.
"... Oktoba ni ya moto, kwa hiyo inahitaji utulivu," amesema Ahmed.
Mbali na mazoezi, Simba inalenga kutumia kambi hiyo kupata mechi za kirafiki zenye ushindani ili kuwapa wachezaji nafasi ya kurejea kwenye ushindani kabla ya kukutana na Yanga, Oktoba 10.