Chuma Daniel Levy kinavyoondoka Spurs
Muktasari:
- Tangazo lililotolewa Alhamisi jioni na Spurs lilithibitisha kufikia mwisho kwa zama za Levy baada ya kuiongoza klabu hiyo kwa robo karne akifanya kazi ya kuwa mwenyekiti kwenye klabu hiyo ya Ligi Kuu England.
LONDON, ENGLAND: BOSI kubwa Daniel Levy amelazimika kuachana na Tottenham Hotspur baada ya miaka 25 ya kuwa kiongozi kwenye kikosi hicho cha London.
Tangazo lililotolewa Alhamisi jioni na Spurs lilithibitisha kufikia mwisho kwa zama za Levy baada ya kuiongoza klabu hiyo kwa robo karne akifanya kazi ya kuwa mwenyekiti kwenye klabu hiyo ya Ligi Kuu England.
Kuondoka kwa Levy, 63, kunadaiwa kumetokana na uchunguzi wa familia ya Lewis ambayo ndiyo inayomiliki hisa nyingi kwenye umiliki wa klabu hiyo.
Tajiri wa Uingereza, bilionea Joe Lewis, 88, alikuwa kiongozi wa kampuni ya ENIC inayoimiliki klabu ya Spurs, lakini sasa kampuni hiyo ipo chini ya watoto wake, Vivienne na Charles, ambao ndiyo waliamua kumfungulia mlango wa kutokea Levy.
Watoto hao wanadaiwa ndiyo wanaofanya mabadiliko makubwa yanayoonekana kwenye kikosi cha Spurs kwa miaka ya karibuni, wakijaribu kuboresha matokeo ya uwanjani. Chini yao wameshuhudia kocha mkuu Ange Postecoglou, ofisa mkuu wa soka Scott Munn na mkurugenzi aliyedumu kwa muda mrefu, Donna Cullen wote wakifunguliwa mlango wa kutokea.
Wakati bosi wa zamani wa Arsenal, Vinai Venkatesham akiwasili Spurs kama mkurugenzi mtendaji mkuu mpya, hilo lilidaiwa ulikuwa mwanzo wa klabu hiyo kujiandaa na maisha baada ya Levy huku Thomas Frank akiletwa kwenye timu hiyo kuwa kocha mkuu.
Na sasa, Peter Charrington amechukua majukumu ya kuwa mwen
yekiti wa klabu hiyo, akimbadili Levy, ambaye ameshinda mataji mawili tu kwa robo karne aliyoongoza timu hiyo, huku moja ya mataji hayo likiwa la Europa League walilobeba Mei, mwaka huu kwa kuichapa Manchester United katika mechi ya fainali iliyopigwa Hispania msimu uliopita.
Charrington alijiunga kwenye bodi ya Spurs, Machi mwaka huu, wakati Venkatesham amekuwa akiwajibika na majukumu ya kila siku ya uendeshaji wa klabu.
Chanzo kutoka kwa mtu wa karibu wa familia ya Lewis kilibainisha: “Kizazi cha familia ya Lewis kimeweka sapoti yake kwenye klabu na wanachotaka ni kilekile kinachotakiwa na mashabiki - kushinda zaidi.
“Hii ndiyo maana kumekuwa na mabadiliko kwa siku za karibuni, uongozi mpya ili kuwa na mambo mapya. Vinai, Thomas na Peter Charrington, wanaaminika kwamba watafanya timu kufikia mafanikio. Hizi ni zama mpya.”€
Familia hiyo ya mmiliki wa klabu ya Spurs, akiwamo mrembo Vivienne, 62 na kaka yake, Charles, 61, watakuwa na wajibu wa kuifanya timu hiyo kuwa moto na hawana mpango wa kuipiga bei.
Kuondoka kwa Levy, ambaye pia ana hisa chache kwenye klabu hiyo iliaminika kwamba kunatoa fursa kwa familia ya Lewis kumiliki hisa zote za klabu hiyo.
Kampuni ya ENIC inamiliki asilimia 86.91 ya hisa za klabu hiyo, wakati Levy aliingia kwenye bodi ya Spurs mwaka 2000 wakati ENIC iliponunua asilimia 27 ya hisa za klabu zilizokuwa chini ya Sir Alan Sugar. Mashabiki wa Spurs ugombi wao na Levy ulikuwa kwenye mataji, ambapo Europa League walibeba baada ya miaka 17 ya kuambulia patupu na taji jingine walilowahi kubeba chini ya uongozi wa bosi huyo ni lile la Kombe la Ligi 2008.
Licha ya mataji kuwa magumu Spurs chini ya Levy bosi huyo ameifanya klabu hiyo kuwa moja ya timu zenye nguvu kwenye Ligi Kuu England.
Ameshuhudia ujenzi wa uwanja wa kisasa kabisa duniani uliofunguliwa 2019 - mwaka ambao Spurs ilifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Levy pia alikuwa mgumu kwenye kuuza wachezaji na alipofanya hivyo, basi alifanya kwa mkwanja ambao ulileta faida kubwa kwa timu ikiwamo kumuuza mchezaji kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia ya uhamisho ya Pauni 85 milioni wakati Gareth Bale alipojiunga na Real Madrid 2013. Chini ya Levy kupata mchezaji Spurs haikuwa rahisi.
Kinachoelezwa pia Spurs ndiyo klabu iliyopata faida kubwa zaidi kwenye Ligi Kuu England kuliko timu zote katika kipindi cha Levy. Timu hiyo ilimuuza Bale kwa pesa nyingi, lakini ilimuuza pia straika Harry Kane kwa Pauni 104 milioni kwenda Bayern Munich.
Kwa ujumla wake, Spurs ilitengeneza faida ya Pauni 167 milioni kwenye kipengele cha kuuza na kununua wachezaji kwenye kikosi cha miamba hiyo ya London.
Timu inayoshika nafasi ya pili kupata faida katika kipindi cha Levy ni Brighton iliyovuna Pauni 102 milioni, wakati Arsenal imepata Pauni 72 milioni na Liverpool Pauni 19 milioni. Kwenye Ligi Kuu England, timu iliyopata hasara kubwa kwenye usajili wakati bosi Levy akiwa Spurs ni Chelsea ambayo imeandikisha hasara ya Pauni 1.257 bilioni. Aston Villa imepata hasara ya Pauni 706 milioni, ikifuatiwa na Everton (Pauni 589 milioni), Manchester City (Pauni 553milioni), Fulham (Pauni 358milioni) na Manchester United (Pauni 261 milioni). Takwimu zinafichua pia chini ya Levy mapato ya Spurs yalipanda kutoka Pauni 48 milioni kwa mwaka hadi Pauni 528 milioni msimu wa 2023-24.
Hilo lilikuwa ongezeko bora kabisa huku akifanikiwa kupunguza bili yao ya mishahara kwa wastani wa kutoka asilimia 52 hadi asilimia 42. Spurs imekuwa timu yenye wastani mdogo wa malipo ya mishahara kwa wachezaji wake kwenye Ligi Kuu England kwa misimu kibao.