Chelsea yajitosa katika vita ya Marc Guehi
Muktasari:
- Guehi ambaye alikulia katika akademi ya Chelsea kabla ya kwenda Palace, alikuwa karibu kujiunga na Liverpool katika dirisha lililopita lakini dili lilifeli dakika za mwisho baada ya kocha wa timu yake kuzuia na kutishia kujiuzuru ikiwa angeuzwa.
CHELSEA imejiunga na timu nyingine za England na Hispania kwa ajili ya kuiwania saini ya beki wa kati wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Marc Guehi, 25, ambaye mkataba wake na Crystal Palace unamalizika mwisho wa msimu huu.
Guehi ambaye alikulia katika akademi ya Chelsea kabla ya kwenda Palace, alikuwa karibu kujiunga na Liverpool katika dirisha lililopita lakini dili lilifeli dakika za mwisho baada ya kocha wa timu yake kuzuia na kutishia kujiuzuru ikiwa angeuzwa.
Palace itahitaji kumuuza fundi huyu dirisha lijalo la majira ya baridi na ikishindikana huenda ikampoteza bure ifikapo mwisho wa msimu.
Guehi amekataa kusaini mkataba mpya ikiwa ni katika kushinikiza kuuzwa jambo ambalo Palace ilikuwa tayari kulifanya kabla ya mambo ya kuvurugika.
Liverpool iliyoonekana kuwa na nafasi kubwa ya kumpata itasubiri hadi mwisho wa msimu na haitowasilisha ofa yoyote ifikapo Januari mwakani.
Bernardo Silva
JUVENTUS wanapanga kumsajili kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Ureno, Bernardo Silva mwenye umri wa miaka 31 kwa uhamisho wa bure mara baada ya mkataba wake kumalizika katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Silva ameichezea Man City tangu 2017 akitokea Monaco na hivi karibuni amekuwa akihusishwa sana kuondoka na mbali ya Juventus, timu yake ya zamani Benfica pia inainyemelea huduma yake.
Kobbie Mainoo
MANCHESTER City inamwinda kiungo wa Manchester United, Kobbie Mainoo, 20, ambaye pia yupo katika rada za Chelsea na Newcastle United. Mainoo amekuwa mmoja wa vijana waliotabiriwa makubwa sana Old Trafford lakini amekuwa na wakati mgumu tangu kuingia kwa kocha mpya Ruben Amorim msimu uliopita ambaye haoni kama anaendana na mifumo yake.
Morgan Rogers
CHELSEA bado inamnyemelea saini ya mshambuliaji wa Aston Villa na England, Morgan Rogers,23, licha ya timu yake kuhitaji zaidi ya Pauni 80 milioni ili kumuuza dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Rogers alisajiliwa na Villa kutoka Middlesbrough mwaka 2024. Mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwaka 2030.
Carlos Baleba
BAADA ya kupata faida katika vyanzo vyao mbalimbali, Manchester United imepata nguvu zaidi ya kufanya mazungumzo kwa ajili ya kumsajili kiungo Brighton na timu ya taifa ya Cameroon, Carlos Baleba mwenye umri wa miaka 21. Baleba alijiunga na Brighton akitokea Lille mwaka 2023 kwa takribani Euro 27 milioni. Msimu uliopita alicheza mechi 30 za Ligi Kuu England.
Christantus Uche
KIUNGO wa Getafe na timu ya taifa ya Nigeria ambaye anacheza kwa Mkopo Crystal Palace, Christantus Uche atasaini mkataba wa kudumu wa kuitumkia Palace ikiwa ataanza katika mechi 10 za michuano yote kwa msimu huu. Staa huyu mwenye umri wa miaka 22, ni miongoni mwa mastaa waliotua Palace dirisha lililopita na mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwakani.
Ronald Araujo
Liverpool ipo tayari kutoa Euro 50 milioni kwa beki kisiki wa Barcelona na timu ya taifa ya Uruguay, Ronald Araujo,26, ambaye Tottenham pia inamnyemelea. Kwa mujibu wa tovuti ya Fichajes, Barca itakuwa tayari kumuuza beki huyu aliyacheza mechi 150 akiwa katika kikosi chao kutokana na changamoto za masuala ya kifedha wanazokumbana nazo. Araujo ni miongoni mwa mabeki bora wa La Liga kwa sasa.
Elliot Anderson
MANCHESTER United imepanga kutuma ofa kwenda Nottingham Forest katika dirisha dogo la Januari kwa ajili ya kumsajili kiungo wa kati wa timu hiyo. Taarifa zinaeleza mchezaji huyo wa kimataifa wa England,22, bado ana furaha ya kuendelea kusalia Nottingham.
Anderson amekuwa mhimili wa safu ya kiungo ya Forest msimu huu. Mkataba wake na Forest unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, na mbali ya Man United saini yake pia inahitajika na Newcastle.