Casemiro ang’ang’ania kuondoka Man United mwisho wa msimu
Muktasari:
- Nyota huyo wa Brazil tayari alitangaza tangu Januari kuwa ataondoka Old Trafford mwisho wa msimu, lakini hivi karibuni kulikuwa na matumaini mapya baada ya Matheus Cunha kusema kuwa bado kuna uwezekano wa kumbadili mawazo.
MANCHESTER, ENGLAND: KIUNGO mkongwe wa Manchester United, Casemiro ameweka wazi hatma yake kwa kusisitiza kuwa hatabadili uamuzi wake wa kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu, licha ya wito kutoka kwa wachezaji wenzake kumtaka abaki.
Nyota huyo wa Brazil tayari alitangaza tangu Januari kuwa ataondoka Old Trafford mwisho wa msimu, lakini hivi karibuni kulikuwa na matumaini mapya baada ya Matheus Cunha kusema kuwa bado kuna uwezekano wa kumbadili mawazo.
Hata hivyo, akizungumza na ESPN, Casemiro aliweka msimamo wake wazi akisema: “Sioni nafasi ya kubaki. Hakuna kabisa. Nataka kuondoka kwa heshima, kupitia mlango mkubwa.”
Kiungo huyo amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha kocha Michael Carrick, akitoa mchango mkubwa kwenye eneo la kiungo huku akishirikiana vyema na chipukizi Kobbie Mainoo katikati ya uwanja.
Mashabiki wa United wamekuwa wakimwimbia nyimbo za kumtaka aongeze mwaka mmoja zaidi klabuni hapo, jambo lililogusa hata familia yake, lakini Casemiro anaonekana kubaki na msimamo wake wa kuondoka akiwa bado yupo kwenye kiwango kizuri.
Aliongeza: “Ilikuwa miaka minne mizuri sana. Nitaendelea kuwa shabiki wa Manchester United hapa England lakini ninaamini huu ndio wakati sahihi wa kuondoka.”
Kwa upande wake, Cunha alieleza umuhimu wa Casemiro ndani ya kikosi hicho, akisema uwepo wake unaleta tofauti kubwa na angependa aendelee kubaki, japokuwa alikiri kuwa uamuzi huo si rahisi kubadilika.
Kocha Carrick naye aliwataka mashabiki kufurahia uwepo wa kiungo huyo kwa muda uliosalia, akimsifu kwa uzoefu wake mkubwa na mchango wake ndani ya timu.