CAS kumaliza utata ubingwa Senegal, Morocco kesho
Muktasari:
- Uamuzi huo utakuwa ni ama wa kubariki uamzi wa Kamati za Nidhamu na Rufaa za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuipa ubingwa Morocco au kuirejeshea ubingwa Senegal.
Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) imepanga kesho Jumanne, Novemba 24, 2026 kutoa uamuzi wa sakata la ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Uamuzi huo utakuwa ni ama wa kubariki uamuzi wa Kamati za Nidhamu na Rufaa za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuipa ubingwa Morocco au kuirejeshea ubingwa Senegal.
Majibu hayo yanatolewa baada ya CAS kusikiliza shauri hilo, Oktoba mwaka huu.
Utata wa jambo hilo ulianza baada ya Senegal kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya fainali iliyochezwa Januari 18, 2026.
Hata hivyo wakati mechi hiyo inaendelea, baadhi ya wachezaji wa Senegal walitoka uwanjani na kuelekea vyumbani kwa lengo la kugomea penalti ambayo Morocco walipata.
Hata hivyo, baadaye walirejea uwanjani na Morocco wakakosa penalti hiyo ambayo ilipigwa na Brahim Diaz.
Baada ya mchezo kumalizika, Senegal walipewa kombe na medali za ushindi lakini siku chache baadaye, Kamati ya Nidhamu ya CAF ilitangaza kuivua ubingwa Senegal na kuipa Morocco huku ikiipa ushindi wa mabao 3-0.
Baada ya uamuzi huo, Senegal walikimbilia CAS ambayo mwezi uliopita ilifanya mapitio ya shauri hilo na kuamua kesho Jumanne iwe siku ya kutoa majibu yanayosubiriwa kwa hamu duniani.