Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Carrick: Naelewa shida zenu

CARRICK Pict

Muktasari:

  • Carrick ameyasema hayo wakati United ikiingia katika kipindi kigumu cha msimu, ikiwa na jukumu la kukabiliana na Atletico Madrid katika Uwanja wa Metropolitano mechi itakayopigwa leo, kabla ya kuikabili Leeds United katika Uwanja wa Elland Road, Jumapili.

MADRID, HISPANIA: KOCHA wa Manchester United, Michael Carrick, amekiri kuelewa sababu zinazowafanya mashabiki wa klabu hiyo kutaka mabadiliko makubwa, kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo mwanzoni mwa msimu.

Carrick ameyasema hayo wakati United ikiingia katika kipindi kigumu cha msimu, ikiwa na jukumu la kukabiliana na Atletico Madrid katika Uwanja wa Metropolitano mechi itakayopigwa leo, kabla ya kuikabili Leeds United katika Uwanja wa Elland Road, Jumapili.

Matokeo mabaya ya United, yakiwemo sare ya bao 1-1 dhidi ya Tottenham iliyokuwa imebaki na wachezaji 10, yameongeza presha kwa kikosi hicho. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, klabu hiyo imekuwa na rekodi yake mbaya zaidi baada ya mechi sita za ligi katika kipindi cha miaka 40.

CARR 04

Hata hivyo, Carrick amesema changamoto hizo hazipaswi kuwa sababu ya kupoteza matumaini, akieleza kuwa vipindi vigumu vinaweza kusaidia kubaini watu walio tayari kupambana kwa ajili ya mafanikio ya muda mrefu ya klabu. “Ninapenda kipindi kama hiki. Wakati mambo hayaendi vizuri, unaona nani hasa yupo pamoja nawe. Unaona ndani ya kikosi, wachezaji na klabu kwa ujumla, nani anataka kubaki kwa muda mrefu na nani anayejali kweli,” amesema Carrick.

Ameongeza kuwa mashabiki wa United bado wana matumaini makubwa na wanahitaji kuona timu yao ikitoa matokeo yanayoridhisha.

“Wafuasi wetu wapo pamoja nasi na wanatamani sana mafanikio. Tunapaswa kuwapa kitu cha kuwafurahisha. Lazima tukubali changamoto ili kufika tunapotaka. Tupo katikati ya kipindi kigumu, lakini ninaamini tutakivuka,” amesema.

CARR 03

Carrick ametumia mifano ya makocha Sir Alex Ferguson na Diego Simeone kueleza umuhimu wa kujenga mafanikio ya muda mrefu, akibainisha kuwa safari ya kuifanya klabu kuwa bora haiwezi kukosa vikwazo.

Simeone amekuwa akiiongoza Atletico Madrid kwa miaka 15, huku Ferguson akiweka historia kubwa akiwa Manchester United kwa miaka 22.

Carrick amesema makocha hao waliweza kujenga misingi imara katika klabu zao licha ya kukutana na vipindi ambavyo mambo hayakwenda kama walivyotarajia.

“Tunazungumzia Sir Alex Ferguson na Diego Simeone, ambao wamejenga kitu cha kipekee katika klabu zao. Kujenga mafanikio katika soka ni safari, na lazima ukabiliane na changamoto mbalimbali,” amesema.

Akizungumzia wito wa mashabiki wa kutaka mabadiliko kila timu inapopata matokeo mabaya, Carrick amesema anaelewa hisia hizo, lakini si njia ambayo United inapaswa kufuata kwa sasa.

CARR 02

“Ninaelewa mambo yasipoenda vizuri, watu wanataka mabadiliko na kuhisi kuwa kila kitu ni janga. Ninaelewa hilo, lakini si mtazamo tulionao sisi. Ili kufikia mafanikio, lazima uweze kukabiliana na mambo magumu na kuyashinda,” amesisitiza.

Alipoulizwa kama anahisi presha kutokana na hali ya timu, Carrick amesema haangalii sana yanayosemwa nje ya klabu, akisisitiza kuwa amepitia nyakati nzuri na mbaya katika maisha yake ya soka.

“Kwangu mimi, hili ni changamoto ninayotaka kuikabili. Ninafurahia kufikiria mambo tunayoweza kuyafanikisha,” amesema.


CARR 01

MAJERUHI YAONGEZA SHIDA

Wakati Carrick akijaribu kutafuta namna ya kuirejesha United kwenye mstari wa ushindi, majeruhi yameendelea kumpa maumivu ya kichwa.

Klabu hiyo ilisafiri kwenda Madrid bila kiungo Kobbie Mainoo na beki Luke Shaw, ambao wote walikosa mazoezi yaliyofanyika Carrington Jumatatu.

Hali ya Shaw ni pigo kubwa zaidi kwa United, hasa ikizingatiwa kuwa klabu hiyo haikusajili beki wa kushoto wa ziada katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi.

Wachezaji waliowahi kuchukua nafasi yake, Patrick Dorgu na Noussair Mazraoui, nao kwa sasa hawapo fiti kucheza. Hali hiyo inamwacha Carrick akifikiria kumtumia beki wa kulia Diogo Dalot au kijana Harry Amass katika eneo hilo dhidi ya Atletico.

Changamoto nyingine ipo kwenye safu ya ushambuliaji, ambako United imejikuta ikilazimika kubadilisha mipango yake kutokana na kutopatikana kwa Benjamin Sesko, aliyepata tena tatizo la jeraha la mfupa wa muundi.

Hata hivyo, beki Matthijs De Ligt alijumuishwa katika kikosi kilichosafiri kwenda Madrid, licha ya kutokuwa amepata nafasi ya kucheza kwa kipindi kirefu.