Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Carrick: Sijahisi kusalitiwa Manchester United

CARRICK Pict

Muktasari:

  • Kwa mara ya pili mfululizo katika michezo ya Ligi Kuu England iliyochezwa nyumbani, United imeshindwa kutumia vyema faida ya kuwa na wachezaji wengi baada ya wapinzani wake kupungu kwa kadi nyekundu.

LONDON, ENGLAND: MANCHESTER United imeendelea kujikuta kwenye wakati mgumu baada ya kushindwa kuifunga Tottenham iliyobaki na wachezaji 10, matokeo yaliyoongeza presha kwa kocha Michael Carrick na hatma ya timu hiyo.

Kwa mara ya pili mfululizo katika michezo ya Ligi Kuu England iliyochezwa nyumbani, United imeshindwa kutumia vyema faida ya kuwa na wachezaji wengi baada ya wapinzani wake kupungu kwa kadi nyekundu.

Pia, kwa mara ya tatu katika misimu mitatu mfululizo, kocha wa United amejikuta akipambana na presha kubwa kabla hata ya majira ya saa kurudishwa nyuma nchini England.

Wiki nne zilizopita, Manchester City ilihitaji uamuzi wenye utata wa mwamuzi msaidizi wa video (VAR) ili kunufaika na kiwango kisichoridhisha cha United, baada ya Phil Foden kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 23 kwa kumkanyaga Bruno Fernandes kwa makusudi.

Jumamosi, United ilijiumiza yenyewe. Tottenham, ambayo ilionekana kushindwa kupata bao kabla ya Rodrigo Bentancur kumpiga kichwa Luke Shaw dakika tano tu baada ya Bryan Mbeumo kuifungia United la kuongoza, kabla ya Spurs kusawazisha katika dakika za nyongeza.

Beki wa kati Lisandro Martinez alishindwa kumzuia Dominic Solanke, huku kipa Senne Lammens akishindwa kusoma vyema mguso wa mshambuliaji huyo ulioufanya mpira kuelekea kona ya mbali na kuingia wavuni.

Nyuso za wachezaji wa United baada ya bao hilo zilieleza wazi namna walivyokuwa wamekata tamaa.

CARR 01

“Siku yenye kutia wasiwasi kwa Michael Carrick,” amesema nahodha wa zamani wa United, Gary Neville, akichambua mchezo huo kupitia Sky Sports.

Kikosi cha Carrick sasa kimecheza mechi nne za ligi bila ushindi na kinatarajiwa kusafiri kukabiliana na mpinzani wake wa jadi Leeds United, kwenye Uwanja wa Elland Road, Jumapili, Oktoba 18.

Kabla na baada ya mchezo huo, United pia inakabiliwa na safari ngumu za Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid na Como.

Viongozi wa United wameendelea kuonyesha kumuunga mkono Carrick katika wiki za hivi karibuni.

Hata hivyo, mashabiki hawajasahau kuwa misimu miwili iliyopita, mfululizo wa ushindi mara mbili pekee katika mechi tisa za mashindano yote ulimweka Erik ten Hag kwenye presha kubwa, kabla ya kufutwa kazi baada ya kipigo dhidi ya West Ham Oktoba 27.

Msimu uliopita, kutolewa kwa United katika Kombe la EFL na Grimsby, inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, pamoja na kipigo cha mabao 3-1 dhidi ya Brentford Septemba 27, kulidhoofisha zaidi imani kwa Ruben Amorim kabla ya kutimuliwa Januari 5. Sasa mwanzo wa msimu huu unaanza kufanana na hali hizo za nyuma.


CARR 04

'SIJAHISI KUSALITIWA'

“Sijafurahishwa na idadi ya pointi tulizopata hadi sasa, hilo ni wazi,” amesema Carrick.

“Sijaribu kulikwepa hilo. Nafikiri mambo yangeweza kuwa tofauti kama tungekuwa makini katika baadhi ya vipengele vidogo, lakini ukweli ndio huo na lazima tukubaliane nao. Tunahitaji kubadilisha mwelekeo na kuanza kupata matokeo mazuri haraka.”

Mambo hayo madogo aliyoyataja Carrick ni pamoja na namna walivyoshindwa kumzuia Solanke kufunga bao la kusawazisha, kushindwa kumkaba Ainsley Maitland-Niles wa Everton alipofunga bao jingine la kusawazisha dakika za mwisho kwenye Uwanja wa Hill Dickinson Septemba 6, na bao la kujifunga la Martinez lililokaribia kuipa Fulham ushindi Craven Cottage kabla ya mapumziko ya mechi za kimataifa.

“Tunapaswa kuwa wajanja zaidi katika nyakati muhimu, kuwa wagumu zaidi na kuonyesha uimara wa kulinda matokeo,” ameongeza.

Carrick alisisitiza kuwa matokeo hayo hayajabadilisha imani yake kwa wachezaji wake, akisema anaamini kikosi hicho kina uwezo wa kufanya vizuri, lakini kinahitaji kuanza kukusanya pointi zaidi.

CARR 02

“Sijahisi kusalitiwa. Wachezaji wanaweza kufanya makosa.

“Sote tuna viwango tunavyopaswa kufikia. Wachezaji wenyewe wanakubali wanapokosea au jambo linapokwenda kinyume nao.

“Si kwamba kila mtu anaondoka uwanjani na kuendelea na maisha yake kana kwamba kila kitu kiko sawa na tatizo limeachwa kwangu pekee. Sivyo ilivyo. Wachezaji wanajali, hilo ni hakika.

“Sijahisi kwamba wamenisaliti kwa kufanya kosa. Tunapaswa kusaidiana ili kuwa bora zaidi, na ni jukumu langu kuwaongoza na kuwasaidia kuvuka hali hii,” amesema Carrick.

Hata hivyo, kila matokeo mabaya yanapojirudia, imani kwamba United ni timu bora inayoweza kushindana kwa mafanikio inaendelea kupungua.

Baada ya mchezo huo, mjadala mwingine ulijikita kwenye umbali ambao wachezaji wa United walikimbia, licha ya takwimu hizo kushindwa kuwasaidia kupata ushindi.

“Takwimu hazidanganyi. Kila timu inapokukimbia zaidi, kuna tatizo,” amesema mchambuzi wa Sky Sports na nahodha wa zamani wa Tottenham, Jamie Redknapp.

“Tottenham ilikimbia kilomita tano zaidi ya Manchester United. Ni kweli walikuwa na wachezaji 10, lakini hili linatokea katika kila mchezo. Ukiweza kumzidi mpinzani wako kwa nguvu na umbali wa kukimbia, una nafasi nzuri ya kushinda. Sisemi kwamba hawajitumi, lakini wanashindwa katika mapambano ya kimwili.”

Naye kiungo wa zamani wa Tottenham, Danny Murphy, amesema kupitia kipindi cha Match of the Day cha BBC kuwa United ilionekana kukosa nguvu na uwezo wa kutawala eneo la kiungo.

“Manchester United ilionekana kucheza kwa kusuasua. Eneo lao la kiungo haliwezi kutawala michezo. Tatizo ni sehemu ya mbinu na sehemu ya aina ya wachezaji waliopo.

“Sielewi kinachoendelea. Mwishoni mwa msimu uliopita, tuliona United ikiwa na mpangilio mzuri zaidi na ikiwa timu ngumu zaidi kucheza nayo.

“Nafasi zilizoachwa katikati ya uwanja zilikuwa kubwa sana. Kama wangekuwa wanacheza dhidi ya timu yenye uwezo zaidi, wangeshindwa. Wakicheza hivyo dhidi ya timu nzuri, watavuliwa nguo,” amesema.


CARR 03

MASHABIKI WANAANZA KUPOTEZA IMANI

Dalili za baadhi ya mashabiki kupoteza imani zilionekana kutokana na namna walivyoitikia matukio mbalimbali ya mchezo, mbali na kuzomea kulikosikika mwishoni mwa kila kipindi.

Mshambuliaji Matheus Cunha, ambaye ni miongoni mwa wachezaji wa kikosi cha Carrick walioshindwa kurejesha kiwango walichoonyesha katika nusu ya pili ya msimu uliopita, alionekana kutoa ishara kwa mashabiki katika kipindi cha kwanza.

Haikufahamika wazi kama alikuwa akijibu maneno ya kukosoa au kuwahamasisha mashabiki kuongeza sauti za kushangilia, lakini ni dhahiri Mbrazil huyo hakuwa na furaha.

Familia ya Carrick ni miongoni mwa wamiliki wa tiketi za msimu za United, hivyo kocha huyo anafahamu hisia za mashabiki wanapoiona timu yao ikipambana na matokeo mabaya kwenye Uwanja wa Old Trafford.

“Ni wazi kwamba inaumiza. Inaumiza sana na si jambo zuri kupitia hali kama hii. Ninaijali klabu hii kama mtu mwingine yeyote. Wakati mwingine unaweza kusema ninaijali kupita kiasi kwa sababu hisia zinaweza kunizidi, lakini yote yanatokana na nia njema, hivyo ninaelewa hali hiyo,” amesema.

Katika nyakati kama hizi, Carrick ambaye kwa kawaida huonekana mtulivu anapozungumza hadharani, anaweza kuwa akipitia msongo mkubwa wa mawazo.

Anafahamu namna presha inavyoweza kuongezeka Old Trafford na jinsi mjadala kuhusu matatizo ya klabu hiyo unavyoweza kuwa mkali wakati mashabiki wakitafuta majibu.