Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Carrick aondoka Man United bila kinyongo

Muktasari:

  • Carrick anatarajiwa kubadilishwa na Mauricio Pochettino, baada ya mwanzo mbaya wa msimu kuifanya Manchester United kuingia katika mapumziko ya mechi za kimataifa ikiwa ndani ya eneo la kushuka daraja.

LONDON, England: KOCHA Michael Carrick ameondoka rasmi Manchester United, lakini ameonyesha kutokuwa na kinyongo na klabu hiyo aliyokuwa sehemu muhimu ya maisha yake akiwa mchezaji na kocha.

Carrick anatarajiwa kubadilishwa na Mauricio Pochettino, baada ya mwanzo mbaya wa msimu kuifanya Manchester United kuingia katika mapumziko ya mechi za kimataifa ikiwa ndani ya eneo la kushuka daraja.

Nyota huyo wa zamani wa United, ambaye aliwahi kuitumikia klabu hiyo akiwa mchezaji, ametoa salamu za kuaga zenye kugusa hisia kwa mashabiki, baada ya pia kuwaaga wachezaji katika mazingira ya kihisia siku iliyotangulia.

Katika ujumbe wake wa kuaga, Carrick alisema ilikuwa heshima kubwa kwake kupewa nafasi ya kuiongoza Manchester United, klabu ambayo anaipenda na yenye historia ya kipekee katika soka.

“Nimepata heshima kubwa ya kuiongoza Manchester United, klabu ya soka ninayoipenda. Ni watu wachache sana wanaopata nafasi ya kuishi na kuhisi jambo kama hilo, na kwa hilo ninashukuru sana.

“Kuiongoza klabu hii kunaambatana na jukumu kubwa. Ukiwa Manchester United, unatakiwa kuelewa kikamilifu maana ya kuwa sehemu ya klabu hii. Ni tofauti na sehemu nyingine yoyote.

“Unapaswa kujitahidi kuwa bora zaidi, lakini pia kuna utamaduni, misingi na mwenendo ambao unatakiwa kuuheshimu na kuufuata. Mambo hayo yamejengwa kwa kipindi kirefu.

“Ni klabu ya kipekee yenye msingi na historia ambayo haiwezi kupuuzwa. Hicho ndicho kilichonipa msukumo kila siku,” alisema.

Carrick pia alitumia nafasi hiyo kuwashukuru mashabiki wa Manchester United, akieleza namna walivyompa upendo na sapoti licha ya matokeo yasiyoridhisha ya timu katika kipindi cha hivi karibuni.

“Nataka kuwashukuru sana mashabiki. Kwa kweli, nyinyi ni wa kipekee na wa aina ya pekee.

“Tumeishi nyakati nzuri mwaka huu ambazo sote tutazikumbuka. Jambo zuri zaidi katika nafasi yangu lilikuwa kuwaona wengi wenu mkizama katika furaha na hisia za nyakati hizo, kisha kuondoka uwanjani mkiwa na hamu ya kurejea tena.

“Nilitaka tu kuwalipa kwa namna fulani. Upendo huo hautakufa kamwe.

“Najua matokeo yetu hayajawa mazuri hivi karibuni, lakini hamjaacha kunionyesha upendo na kuniunga mkono, wakati ambapo jambo rahisi zaidi kwa wengi lingekuwa kugeuka na kuondoka.

“Hilo lina maana kubwa zaidi ya ushindi mmoja au miwili. Ndilo linalowafanya kuwa mashabiki mlivyo. Ndiyo sababu niliipenda klabu hii miaka mingi iliyopita,” alisema.

Aidha, Carrick aliwashukuru makocha wasaidizi na wafanyakazi wengine wa klabu hiyo kwa mchango wao katika kipindi chote alichokuwa akifanya kazi nao, huku akiwatakia kila la heri wachezaji katika safari yao inayofuata.

“Shukrani za pekee kwa benchi langu la ufundi. Kila siku mlinipa kila kitu mlichokuwa nacho, na sikuweza kuomba zaidi ya hapo. Ninashukuru sana kwa uaminifu, bidii na sapoti yenu.

“Kwa wafanyakazi wote wanaofanya kazi nyuma ya pazia, asanteni kwa kila mnachokifanya kwa ajili ya klabu hii. Kazi nyingi mnazofanya hazionekani, lakini mchango wenu hautapuuzwa.

“Kwa wachezaji, asanteni kwa juhudi zenu na nyakati tulizoshiriki pamoja. Naw takia kila la heri katika yale yanayowasubiri,” alisema.

Akihitimisha ujumbe wake, Carrick alisema ataendelea kuitakia mafanikio Manchester United kwa kuwa klabu hiyo imekuwa sehemu kubwa ya maisha yake na kwamba ataendelea kuiunga mkono hata baada ya kuondoka kwenye nafasi ya ukocha.

“Ninaitakia Manchester United mafanikio pekee. Klabu hii imekuwa sehemu kubwa sana ya maisha yangu na hilo halitabadilika kamwe.

“Nitaendelea kujivunia mchango wangu katika klabu hii na daima nitaitakia mema. Kuanzia sasa nitakuwa pamoja nanyi, nikitazama pembeni mwa uwanja na kuwashangilia vijana,” alisema.