Carrick aingia mtego wa Solskjaer, Man United yakumbuka historia
Muktasari:
- Carrick alipewa nafasi ya kuiongoza United baada ya Ruben Amorim kuondolewa, akifuata njia iliyowahi kutumiwa na Solskjaer aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya Jose Mourinho. Wote walikuwa wachezaji waliokuwa na heshima kubwa Old Trafford na walipewa jukumu la kuibadilisha timu baada ya kocha wa kigeni kuondoka.
MANCHESTER, ENGLAND: PRESHA inaanza kumwandama kocha wa Manchester United, Michael Carrick, baada ya uongozi wa klabu hiyo kuanza kukabiliwa na wasiwasi kuhusu mwenendo wa timu, huku historia ya Ole Gunnar Solskjaer ikianza kujirudia.
Carrick alipewa nafasi ya kuiongoza United baada ya Ruben Amorim kuondolewa, akifuata njia iliyowahi kutumiwa na Solskjaer aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya Jose Mourinho. Wote walikuwa wachezaji waliokuwa na heshima kubwa Old Trafford na walipewa jukumu la kuibadilisha timu baada ya kocha wa kigeni kuondoka.
Solskjaer alianza vizuri akiwa kocha wa muda na baadaye akapewa mkataba wa kudumu, lakini mambo yalibadilika matokeo yalipoanza kushuka na presha kuongezeka.
Hali hiyo sasa inatajwa kuwa tahadhari kwa Carrick, ambaye ameshuhudia United ikipoteza mechi mbili kati ya nne za Ligi Kuu kabla ya kuondolewa kwenye Kombe la Carabao baada ya kupoteza uongozi wa mabao 2-0 dhidi ya Brighton.
Uongozi wa klabu, ukiongozwa na kundi la INEOS linalosimamia masuala ya soka pamoja na familia ya Glazer, unatakiwa kuwa na wasiwasi kutokana na mwenendo huo, ingawa bado ni mapema katika msimu kuanza kufikiria mabadiliko ya kocha.
Miaka takribani mitano iliyopita, Solskjaer alifikia mwisho wa safari yake baada ya United kuchapwa mabao 4-1 na Watford Novemba 2021, ikiwa ni kipigo chake cha nne katika mechi tano.
Baada ya kipigo hicho, uongozi wa United uliitisha kikao cha dharura kilichodumu kwa saa kadhaa, kabla ya Joel Glazer kuidhinisha uamuzi wa kumuondoa Solskjaer.
Sasa Carrick anahitaji ushindi katika mchezo ujao dhidi ya Fulham kabla ya mapumziko marefu ya mechi za kimataifa kuanza baada ya mchezo huo.
Ingawa Carrick amesema hajisikii kuwa yuko kwenye presha, amekiri kuwa ukosoaji kutoka nje umeongezeka baada ya kipigo dhidi ya Brighton.
Kocha huyo amesisitiza kuwa timu yake bado inaweza kubadilisha hali hiyo, akisema wachezaji wana uwezo wa kufanya hivyo.
“Bila shaka tunaweza kubadilisha hali hii. Tuna wachezaji wazuri sana na hali inaonekana kuwa mbaya kwa sasa kwa sababu hatujawa na wiki nzuri, au wiki mbili au tatu nzuri,” amesema Carrick.
Ameongeza kuwa matokeo ya nyuma hayana umuhimu mkubwa kama kile ambacho timu itafanya katika mchezo unaofuata.
“Daima ni kuhusu kitakachotokea baadaye. Unachofanya sasa na utakachofanya baadaye. Hilo ndilo changamoto kubwa. Imekuwa hivyo hapa na itaendelea kuwa hivyo,” amesema.
Hata hivyo, kutokana na namna mambo yalivyokwenda kwa Solskjaer, Carrick hawezi kujisikia salama licha ya heshima kubwa aliyonayo Old Trafford.