Carrick afichua kilichomkwamisha huko Goodison Park
Muktasari:
- United walionekana kuelekea kwenye ushindi baada ya mshambuliaji Benjamin Sesko kuifungia timu hiyo bao la pili dakika ya 88, lakini Ainsley Maitland-Niles aliharibu sherehe hizo kwa kufunga bao la kusawazisha dakika za mwisho kabisa.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Manchester United, Michael Carrick, amekiri kuwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Everton ilimfanya ajisikie kana kwamba timu yake imepoteza mchezo, baada ya wenyeji kusawazisha katika dakika ya mwisho ya muda wa nyongeza.
United walionekana kuelekea kwenye ushindi baada ya mshambuliaji Benjamin Sesko kuifungia timu hiyo bao la pili dakika ya 88, lakini Ainsley Maitland-Niles aliharibu sherehe hizo kwa kufunga bao la kusawazisha dakika za mwisho kabisa.
Bao hilo lilikuwa tamu zaidi kwa Maitland-Niles, ambaye alikuwa akiichezea Everton kwa mara ya kwanza baada ya kujiunga na klabu hiyo kutoka Lyon kwa ada ya pauni 4.2 milioni siku ya mwisho ya usajili.
Carrick hakuficha masikitiko yake baada ya mchezo huo.
“Tumekatishwa tamaa sana. Nahisi kama tumepoteza. Tumepata pointi moja na hatuwezi kuipuuza, lakini tunahisi tulipaswa kupata zaidi,” amesema.
United walitangulia kupitia Bryan Mbeumo muda mfupi baada ya mapumziko, kabla ya Tyrique George kuisawazishia Everton kwa shuti kali.
Sesko kisha aliwapa wageni matumaini ya ushindi kwa kufunga bao la pili kwa kichwa, lakini Maitland-Niles akamalizia kazi kwa shuti kali lililojaa kwenye kona ya juu ya lango na kuifanya Everton ipate pointi moja.
CARRICK ALIA NA MABEKI
Sare hiyo imeifanya Manchester United kuruhusu mabao mawili katika kila mchezo wao mitatu ya mwanzo ya msimu dhidi ya Hull City, Ipswich Town na sasa Everton, huku wakikusanya jumla ya pointi nne.
Hata hivyo, Carrick amesema haamini kwamba mwanzo wa msimu umekuwa mbaya, lakini amekiri wazi kuwa safu yake ya ulinzi inahitaji kubadilika.
“Hatujaanza msimu vibaya kiasi hicho. Leo tulikuwa karibu sana kuondoka na pointi tatu. Kuna nyakati tungeweza kufanya vizuri zaidi, lakini tutakuwa sawa nafikiri kuna sehemu kwenye ulinzi kunahitaji maboresho,” amesema.
Carrick ameongeza: “Hatuwezi kupuuza hilo. Tunahitaji kuruhusu mabao machache ili kuongeza nafasi ya kushinda michezo. Tutaangalia hilo na kuendelea kuboresha.”
Kocha huyo pia alieleza kuwa mabao ya Everton yalitokana zaidi na mashuti mazuri ya mbali, akisema si kila mara aina hiyo ya mashuti huishia golini.
RASHFORD APATA PIGO
Marcus Rashford alikuwa miongoni mwa wachezaji walioonyesha kiwango kizuri kwa United, lakini alilazimika kutolewa kipindi cha pili baada ya kuonekana kushika sehemu ya nyuma ya paja lake.
Carrick amesema Rashford alikuwa akihisi maumivu madogo na akaamua kumtoa.
“Alikuwa akihisi kitu kidogo. Alionekana kuwa fiti na mwenye hatari tena, lakini nafasi ya mwisho haikumwangukia,” amesema Carrick.
MAITLAND NILES ACHEKELEA
Wakati Carrick akitoka uwanjani akiwa amevunjika moyo, upande wa Everton ulikuwa kwenye shangwe kubwa baada ya bao la dakika za mwisho.
Maitland-Niles, ambaye alikuwa ametimiza uhamisho wake kwenda Everton siku tano zilizopita, amesema bao hilo lilimpa hisia za ushindi.
“Nilijisikia kama ushindi. Ni jambo la kushangaza. Kila mtu anataka kuanza hivi na kwa bahati nilifanikiwa,” amesema.
Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal alieleza jinsi alivyofunga bao hilo:
“Mpira uliniangukia pembeni mwa boksi, nikaupiga kwa nguvu na ukaenda moja kwa moja kwenye kona ya juu. Ninafurahi sana.”
Amesema Everton walipambana hadi mwisho kwa msaada wa mashabiki wao.
“Tulipambana kwa nguvu na tukafanikiwa kupata pointi. Mashabiki walikuwa pamoja nasi na tulipigana hadi mwisho. Ndiyo maana unapata matokeo kama haya.”