Cape Verde yatoa onyo kwa vigogo WAFCON
Muktasari:
- Martins alisema kikosi hicho kinaweza kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano hayo kwani wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaweka historia.
MSHAMBULIAJI wa timu ya taifa ya Cape Verde, Sandra Martins watu hawapaswi kuwabeza kutokana na ugeni wao kwenye mashindano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) yanayoendelea nchini Morocco.
Martins alisema kikosi hicho kinaweza kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano hayo kwani wamejipanga vizuri kuhakikisha wanaweka historia.
Aliongeza kuwa kitendo cha kucheza WAFCON ni mafanikio makubwa na kwamba kikosi hicho kina uwezo wa kufanya makubwa.
“Nadhani tutafanya vizuri, labda hata zaidi ya watu wanavyotegemea licha ya ugeni wetu. Tunalenga kushinda mechi mbili na ikiwezekana kufuzu robo fainali. Kama kila mmoja atajitoa na tukafanya kazi kama timu, tuna nafasi ya kutinga hatua inayofuata,” alisema Martins na kuongeza
“Tumekuja kushindana hivyo hatutakata tamaa tutapambana kuhakikisha tunaandika historia kwenye fainali hizo kwa hiyo hatujaja kinyonge.”
Kauli hiyo inaonyesha kuwa lengo la Cape Verde siyo kushiriki tu mashindano bali ni kuvuka hatua ya makundi. Ikiwa watafanikiwa kushinda angalau mechi mbili kama walivyojiwekea mapengo, watajiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali na kuandika historia nyingine katika ushiriki wao wa kwanza.
Cape Verde imepangwa Kundi D pamoja na Ghana, Cameroon na Mali, kundi ambalo linatajwa kuwa gumu kutokana na na uzoefu mkubwa wa wapinzani wake katika mashindano ya CAF.
Kwenye kundi hilo, Cameroon ndiyo timu yenye historia kubwa zaidi kwenye kundi hilo. Iliwahi kufika fainali ya WAFCON mwaka 2016 ilipoandaa mashindano hayo nyumbani kabla ya kupoteza 1-0 dhidi ya Nigeria.
Ghana ni moja ya mataifa yenye historia kubwa katika soka la wanawake Afrika, ikiwa imewahi kucheza fainali za WAFCON mara tatu (1998, 2002 na 2006) na Mali ambayo imeendelea kukua kwa miaka ya hivi karibuni.