CAF yachukua tahadhari pambano la MC Alger, Rangers
Picha na Mtandao
Muktasari:
- CAF imemteua mtaalamu wa masuala ya usalama kutoka Uganda, Dixon Okello, kusimamia masuala ya usalama katika mchezo huo utakaochezwa nchini Algeria Ijumaa, Oktoba 23, 2026.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limechukua tahadhari za ziada za kiusalama kuelekea mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya MC Alger ya Algeria na Rangers International ya Nigeria, baada ya matukio yaliyojitokeza katika pambano la kwanza.
CAF imemteua mtaalamu wa masuala ya usalama kutoka Uganda, Dixon Okello, kusimamia masuala ya usalama katika mchezo huo utakaochezwa nchini Algeria Ijumaa, Oktoba 23, 2026.
Uteuzi wa Okello ni sehemu ya hatua za ziada za kiusalama ambazo CAF imeamua kuchukua kutokana na hali ya mvutano inayozunguka mchezo huo, ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa huku timu zote zikipambana kusaka nafasi ya kusonga mbele katika mashindano hayo.
Hatua hiyo inatokana na kitendo cha mashabiki wa MC Alger kufanya vurugu baada ya timu yao kupoteza dhidi ya Rangers International ya Nigeria katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, uliochezwa nchini Nigeria.
Picha na Mtandao
Katika mchezo huo, uliochezwa Oktoba 18, 2026, kwenye Uwanja wa MKO Abiola, Abeokuta, Nigeria, Rangers International iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya MC Alger.
Ushindi huo uliipa timu hiyo ya Nigeria faida muhimu kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa nchini Algeria.
Vurugu hizo zilihusisha uharibifu wa mali za uwanja, ikiwemo kuvunjwa kwa uzio, hali iliyozua wasiwasi kuhusu usalama kuelekea mchezo wa marudiano nchini Algeria na kuifanya CAF kuongeza tahadhari za kiusalama kwa pambano hilo.
Rangers ilipata ushindi huo licha ya kucheza ikiwa na wachezaji 10 kuanzia dakika ya 13 baada ya kipa wake, Lucky Jimoh, kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumchezea faulo mshambuliaji wa MC Alger, Zakaria Naidji.
Picha na Mtandao
Hata hivyo, MC Alger nayo ilipunguzwa idadi ya wachezaji baada ya beki wake, Oussama Benhaoua, kuonyeshwa kadi nyekundu katika kipindi cha pili baada ya kupata kadi ya pili ya njano
Baada ya pande zote mbili kubaki na wachezaji 10, Rangers ilitumia vyema nafasi zilizopatikana na kupata bao la kwanza kupitia kwa Kenneth Igboke, aliyefunga kwa mkwaju wa penalti dakika ya 84.
Dakika tatu baadaye, James Emo aliongeza bao la pili na kuipa Rangers ushindi wa mabao 2-0, matokeo yanayoifanya MC Alger kuwa na kazi ya ziada katika mchezo wa nyumbani.
MC Alger sasa italazimika kushinda kwa tofauti ya angalau mabao matatu ili kupata ushindi wa jumla ndani ya dakika 90, ili ifuzu moja kwa moja.
Picha na Mtandao
Kwa upande wa Rangers, sare au ushindi wowote nchini Algeria utaifanya isonge mbele.
Kutokana na ushindani na matukio ya mchezo wa kwanza, hatua za CAF kuimarisha usimamizi wa usalama zinaonyesha umuhimu wa kuhakikisha mchezo wa marudiano unafanyika katika mazingira salama kwa wachezaji, benchi za ufundi, viongozi na mashabiki.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa wa presha kubwa kwa MC Alger, inayotafuta kurejesha matumaini mbele ya mashabiki wake, huku Rangers ikilenga kulinda faida ya mabao mawili ili kusonga mbele katika Ligi ya Mabingwa Afrika.