Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bruno Fernandes kubaki Old Trafford? Man United yaanza mazungumzo

Muktasari:

  • Vyanzo vimethibitisha kuwa mazungumzo ya awali tayari yamefanyika kati ya klabu hiyo na wawakilishi wa Fernandes, huku United ikitaka kuhakikisha nahodha wake anaendelea kuitumikia timu hiyo katika dimba la Old Trafford chini ya mkataba mpya.

MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United imefungua rasmi mazungumzo na nahodha wake Bruno Fernandes kuhusu mkataba mpya, ikiwa na lengo la kumfunga kiungo huyo anayeonekana kuwa mhimili muhimu wa kikosi hicho kwa muda mrefu zaidi.

Vyanzo vimethibitisha kuwa mazungumzo ya awali tayari yamefanyika kati ya klabu hiyo na wawakilishi wa Fernandes, huku United ikitaka kuhakikisha nahodha wake anaendelea kuitumikia timu hiyo katika dimba la Old Trafford chini ya mkataba mpya.

Nyota huyo wa kimataifa wa Ureno amebakiwa na miezi 10 kwenye mkataba wake wa sasa wenye thamani ya mshahara wa Pauni 220,000 kwa wiki, ingawa Manchester United ina kipengele kinachoiwezesha kuongeza mkataba huo kwa mwaka mwingine.

Licha ya kuibuka kwa tetesi mpya kuhusu hatma ya Fernandes katika kipindi hiki cha kiangazi, Manchester United imesisitiza kuwa inataka kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31 abaki klabuni hapo na inatarajia kufikia makubaliano mapya kabla ya mwisho wa mwaka.

Fernandes alionyesha tena umuhimu wake ndani ya kikosi cha Michael Carrick Jumapili iliyopita, alipofunga hat-trick na kutoa asisti moja katika ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Ipswich, katika wiki ambayo pia alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA.


TAKWIMU ZAKE

Fernandes, aliyewahi kuichezea Sporting Lisbon, amefunga mabao 110 na kutoa asisti 109 katika mechi 329 alizoichezea Manchester United tangu alipohamia Old Trafford mwaka 2020.

Akizungumza wiki iliyopita, kiungo huyo alisisitiza kwamba anatamani kubaki Manchester United na kuendelea kucheza katika kiwango cha juu zaidi, baada ya kuweka rekodi ya Ligi Kuu England msimu uliopita kwa kutoa asisti 21.

Fernandes alisema:

“Kwangu ni suala la kuwa bora kadiri ninavyoweza ili niendelee kucheza pamoja na walio bora  na kucheza na walio bora ni kucheza kwenye Premier League na kuichezea Man United.”

Aliongeza:

“Malengo na kila kitu ninachojiwekea kwa msimu wangu kila mwaka huwa ni kilekile. Sibadiliki, na mambo hayo hayabadiliki kwa sababu nimekuwa hapa kwa kipindi kirefu au kifupi.”

Fernandes pia alieleza kuwa yuko tayari kucheza kwa namna ambayo kocha anamhitaji, huku akisisitiza kwamba kama atashindwa kufikia kiwango kinachohitajika, atalazimika kupisha wengine.

“Nacheza kwa nguvu na kwa kiwango ambacho meneja anahitaji nicheze, na kama sitakuwa na uwezo au sitaweza kufanya hivyo, ninahitaji kupisha. Nafikiri kila mchezaji anahitaji kuelewa muda wake, nyakati zake na wakati wake.”


GALATASARAY YAMVUTIA

Fernandes ameibuka kuwa mchezaji anayewindwa na Galatasaray katika kipindi hiki cha kiangazi, huku klabu hiyo ya Uturuki ikiwa tayari kumpa mkataba wa miaka minne ambao ungemfanya alipwe mshahara mara mbili ya anaoupata sasa.

Mbali na mshahara huo mkubwa, Galatasaray pia iko tayari kumpa Fernandes Pauni 3.5 milioni kama ada ya kusaini mkataba.

Klabu za Juventus na AC Milan nazo zimeripotiwa kufuatilia kwa karibu hali ya mchezaji huyo huko Old Trafford, ingawa kipengele cha mkataba wake kilichokuwa kikimwezesha kuondoka kwa ada ya Pauni 56.7 milioni kilimalizika mwezi Julai.

Hali hiyo inafuatia kipindi cha kiangazi cha mwaka uliopita kilichojaa tetesi za Fernandes kuondoka Manchester United, wakati ambapo alikaribia kujiunga na Al-Hilal ya Saudi Arabia.

Wakala wake, Miguel Pinho, alifanya mazungumzo mjini Riyadh na viongozi wa Al-Hilal, ambao walikuwa tayari kumpa Fernandes mkataba wenye thamani ya takribani Pauni 200 milioni kwa miaka mitatu, huku Manchester United ikiahidiwa ada ya uhamisho ya Pauni milioni 100.