Brighton yaitibulia Man City, Arsenal uwanjani kesho
Muktasari:
Man City inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 21.
Brighton imeipa mshtuko Man City baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) iliyochezwa leo Jumamosi, Oktoba 31, 2026 katika Uwanja wa Etihad, Manchester, England.
Hicho ni kipigo cha pili mfululizo kwa Man City katika EPL, kikitanguliwa na kile cha mabao 2-1 ilichokipata kutoka kwa Aston Villa, Oktoba 20, 2026.
Bao pekee lililoizamisha Man City nyumbani leo limefungwa na Yasin Ayari katika dakika ya 11 akimalizia pasi ya Maxim De Cuyper.
Ushindi huo umeifanya Brighton ilipe kisasi kwa Man City ambayo Jumatano iliyopita iliwatoa katika Kombe la Carabao baada ya kuwafunga kwa mikwaju ya penalti 4-3.
Kwa upande mwingine matokeo hayo yameirudisha Brighton katika mstari wa matokeo mazuri baada ya kupoteza mechi iliyopita ya Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool.
Matokeo hayo yanaipa fursa nzuri Arsenal kukamata kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England kwa vile yameifanya Man City ibakie na pointi zake 21 sawa na zile za Arsenal.
Hata hivyo, Arsenal ina faida ya mechi moja mkononi ambayo itacheza na Liverpool kesho Jumapili katika Uwanja wa Anfield.
Matokeo ya ushindi au sare, yataifanya Arsenal kuipiku Man City na kuongoza msimamo wa EPL.
Kwa sasa, Man City iko juu ya Arsenal ikibebwa na faida ya utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ingawa timu zote mbili kila moja ina pointi 21.
Utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa ya Man City ni 10 na Arsenal ni mabao nane.
MATOKEO YA MECHI ZA LIGI KUU ENGLAND LEO
Chelsea 2-0 Man United
Bournemouth 2-0 Leeds United
Brentford 2-0 Nottingham Forest
Coventry City 3-1 Sunderland
Hull City 2-2 Ipswich Town
Man City 0-1 Brighton