Biashara zafungwa staa akizikwa
Muktasari:
- De Miguel, mwenye umri wa miaka 30, alifariki dunia baada ya kupata ajali ya kugongana na kipa wakati wa mchezo wa soka, tukio lililoitikisa Hispania na kuibua simanzi kubwa kwa wadau wa soka nchini humo.
TENERIFE, HISPANIA: FAMILIA ya mshambuliaji wa klabu ya Tenerife, Jesus de Miguel, imesema kifo cha ghafla cha nyota huyo kimeiacha familia katika majonzi makubwa, huku ikieleza kuwa pengo aliloacha haliwezi kuzibika.
De Miguel, mwenye umri wa miaka 30, alifariki dunia baada ya kupata ajali ya kugongana na kipa wakati wa mchezo wa soka, tukio lililoitikisa Hispania na kuibua simanzi kubwa kwa wadau wa soka nchini humo.
Mamia ya watu walijitokeza katika mji wa Navahermosa, alikozaliwa nyota huyo na ambako familia yake inaishi, kushiriki mazishi yake na kutoa heshima za mwisho.
Mwili wa marehemu uliwasili katika Kanisa la San Miguel Arcángel muda mfupi kabla ya saa 8:00 mchana, ukiwa ndani ya gari aina ya Mercedes-Benz jeusi lililopambwa kwa maua ya waridi nyekundu na ya pinki.
Wazazi wake pamoja na dada yake walifuata gari hilo wakiwa katika huzuni kubwa, huku mpenzi wake akiwafuata nyuma yao.
Mamia ya waombolezaji, wakiwemo wachezaji wenzake wa Tenerife, walishiriki msafara huo uliojazana katika mitaa ya mji huo.
Huzuni ilitawala huku baadhi ya waombolezaji wakishindwa kuzuia machozi, wengine wakiwa wamevalia skafu za klabu ya UD Tenerife kuonesha heshima kwa marehemu.
Kanisa lilifurika kiasi kwamba zaidi ya watu 200 walilazimika kusikiliza ibada wakiwa nje ya jengo hilo.
Ujumbe uliokuwa umeandikwa kwenye bango dogo lililowekwa kwenye maua yaliyopamba gari la kubebea mwili ulisema: “Familia yetu haitakusahau.”
Wakati ibada ikiendelea, shughuli nyingi za kibiashara katika mji huo zilisitishwa, huku maduka na migahawa vikifungwa ili kutoa nafasi kwa wakazi kushiriki maombolezo.
Familia ya marehemu ilitoa hotuba mbalimbali ndani ya kanisa, huku sauti zao zikitetemeka kwa uchungu na baadhi wakishindwa kuzuia machozi.
Kila mmoja alipomaliza kuzungumza, waombolezaji waliokuwa ndani na nje ya kanisa walilipuka kwa makofi kuonesha heshima na upendo wao kwa De Miguel.
Baada ya ibada iliyodumu kwa dakika 75, jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu lilibebwa na ndugu pamoja na marafiki zake kuelekea katika Makaburi ya Manispaa ya Navahermosa, ambako alizikwa.
Wachezaji wenzake walionekana kukumbatiana kwa huzuni huku machozi yakiwatoka baada ya kutoka kanisani.
Vilevile, wawakilishi wa klabu mbalimbali za madaraja ya juu ya soka nchini Hispania waliweka mashada ya maua katika eneo la makaburi, yakiambatana na bango lenye picha ya De Miguel akishangilia bao.
Katika taarifa iliyotolewa na familia yake, kupitia msemaji wao Manuel Hernandez, walisema kifo cha De Miguel kimeacha pengo kubwa lisiloweza kuzibika.
“Jesus ameacha pengo ambalo haliwezekani kuzibwa, lakini pia kumbukumbu kubwa katika mioyo yetu sisi tuliobahatika kushiriki maisha yetu pamoja naye.
“Tunawashukuru wote waliomkumbuka, wachezaji wenzake, marafiki, mashabiki na klabu zote zilizotuma salamu za rambirambi na kuungana nasi katika kipindi hiki kigumu.
“Kuona namna watu wengi walivyompenda Jesus na kutambua athari aliyokuwa nayo katika maisha ya watu wengi ni jambo ambalo tutalibeba mioyoni mwetu daima,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo."
Kifo cha De Miguel kimeacha simanzi kubwa katika familia yake, klabu yake na jamii ya soka nchini Hispania, huku mamia ya watu wakijitokeza kutoa heshima za mwisho kwa nyota huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 30.