Berahino astaafu soka, ageukia ukocha
Nyota wa Burundi, Saido Berahino. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Alicheza mechi 133 za Ligi Kuu England akiwa na timu za West Bromwich na Stoke City na kufunga mabao 23 na katika klabu za Zulte Waregem na Charleroi za Ubelgiji alicheza mechi 51 na kufunga mabao 12.
Baada ya kutumikia soka la ushindani kwa miaka 15, nyota wa Burundi, Saido Berahino amestaafu rasmi kucheza soka la ushindani.
Berahino aliyewahi kucheza Ligi Kuu ya England (EPL) katika klabu ya West Bromwich, amesema anaachana na soka akiwa hana anachodai kwa mchezo huo kutokana na manufaa ya kimaisha ambayo umempatia.
“Mpira wa miguu umenipa kila kitu. Kutoka mitaa ya Bujumbura hadi Hawthorns. Kutoka Ligi Kuu England hadi katika maeneo ambayo sikudhani ningeweza kucheza. Huu mchezo umembeba mtoto mdogo mkimbizi katika maisha.
“Napenda kuishukuru West Bromwich Albion kwa kuniamini wakati nilipokuwa mvulana. Miaka yote klabuni, mabao, mashabiki na nyakati, mara zote zitaendelea kuwa za kipekee.
“Kwa kila mchezaji mwenzangu, kocha na shabiki ambaye ameshiriki katika safari, asante sana.
Nyota wa Burundi, Saido Berahino. Picha na Mtandao
Berahino ameelezea safari yake kisoka kama iliyokumbana na changamoto na nyakati za furaha ambazo zimemfanya asitengane na mchezo huo.
“Kulikuwepo upandaji na kushuka, makosa na mafunzo. Nimejifunza kwamba mchezo unaweza kukupandisha na kukupa kipimo muda huohuo. Katika yote hayo, soka lilibakia palepale kwangu.
“Muda umefika wa kuning’iniza viatu vyangu. Mwili wangu na moyo wangu vipo tayari jwa ukurasa mpya. Naona fahari na nashukuru kwa sasa kuiwakilisha Timu ya Taifa ya Burundi kama Kocha.
“Kurudisha kwa nchi ambayo imenitengeneza na kusaidia kizazi kijacho, najihisi sahihi. Kwa familia yangu, mmekuwa uimara wangu. Kwa mashabiki ambao mlikuwa na mimi katika kila kurasa, sitoweza kusahau sapoti yenu.
“Hii sio kusema kwaheri kwa mpira wa miguu. Kirahisi tu hii ni mwisho wa hadithi moja na mwanzo wa nyingine. Kwa upendo na shukurani,” amesema Berahino.
Nyota wa Burundi, Saido Berahino. Picha na Mtandao
Berahino ameamua kutundika daruga akiwa na umri wa miaka 33 huku akiwa na wasifu wa kucheza katika Ligi Kuu za England (EPL) na Ubelgiji huku pia akiwahi kuchezea timu za taifa za vijana za England kuanzia umri chini ya miaka 16 hadi chini ya miaka 21.
Alicheza mechi 133 za Ligi Kuu England akiwa na timu za West Bromwich na Stoke City na kufunga mabao 23 na katika klabu za Zulte Waregem na Charleroi za Ubelgiji alicheza mechi 51 na kufunga mabao 12.
Berahino anastaafu akiwa ameitumikia timu ya taifa ya Burundi katika mechi 18 na kufunga mabao mawili.