Beki Algeria: Safi AFCON miaka minne
Muktasari:
- Jana timu hizo zilikuwa uwanjani usiku kuamua nani azifuate Misri na Nigeria katika 16 Bora baada ya wapinzani wao hao kukata tiketi kupitia makundi ya B na C kwa kukuvuna pointi sita kila moja.
UAMUZI wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) wa kuandaa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kila baada ya miaka minne imeungwa mkono na beki wa Algeria, Aissa Mandi aliyesema ni hatua chanya itakayolipa thamani zaidi michuano hiyo mikubwa barani humu.
“Kuandaa mashindano kila baada ya miaka minne ni jambo zuri. Ni bora kuliko kila baada ya miaka miwili,” Mandi aliambia waandishi wa habari juzi Jumamosi, siku moja kabla ya mechi ya Kundi E dhidi ya Burkina Faso iliyopigwa usiku wa jana.
“Itafanana na mashindano makubwa ya mabara mengine, kama Mashindano ya Mataifa ya Ulaya (Euro) na hilo lina mantiki na ni jambo jema kwa soka la Afrika kwa ujumla,” aliongeza Mandi.
Uamuzi wa CAF wa kuanza kuandaa AFCON kila baada ya miaka minne kuanzia 2029, uliotangazwa kabla ya michuano ya 2025 inayofanyika Morocco, umezua mjadala mkubwa. Wakosoaji wengi wanasema uamuzi huo unaonyesha kukosa heshima kwa utamaduni wa bara la Afrika wa kuendesha mashindano hayo kila baada ya miaka miwili tangu mwaka 1957.
Kocha wa Mali, Tom Saintfiet, alikuwa mkosoaji mkubwa wa uamuzi huo, akimlaumu Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa mabadiliko hayo.
“Tangu mwaka 1957, Afrika imekuwa ikiandaa Kombe kila baada ya miaka miwili, sasa wanasema kila baada ya miaka minne. Hili si jambo la haki. Afrika lazima iheshimiwe,” amesema kocha huyo wa zamani wa Yanga.
Algeria ilianza kampeni ya msimu huu w AFCON 2025 kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sudan na kuongoza kundi kwa pointi tatu mbele ya Burkina Faso kwa tofauti ya mabao, baada ya Burkina Faso kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Guinea ya Ikweta wakitoka nyuma mwishoni mwa mechi.
Jana timu hizo zilikuwa uwanjani usiku kuamua nani azifuate Misri na Nigeria katika 16 Bora baada ya wapinzani wao hao kukata tiketi kupitia makundi ya B na C kwa kukuvuna pointi sita kila moja.