Bayern yajipanga kumpa mkataba Nicolas Jackson
Muktasari:
- Jackson alisajiliwa na Chelsea kutoka Villarreal kwa Pauni 32 milioni mwaka 2023 lakini baada ya kuona hana nafasi kubwa ya kucheza aliomba kutolewa kwa mkopo kwenda Bayern katika dili lililokuwa karibu kuvunjika baada ya Chelsea kuiambia timu hiyo haina mpango wa kuendelea na mchakato, baada ya Liam Delap kuumia, hivyo walihitaji staa huyo arejee kuziba pengo lake.
BAYERN Munich inajiandaa kumpa mkataba mpya wa muda mrefu mshambuliaji wao wa kimataifa wa Senegal, Nicolas Jackson, 24, ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo katika timu yao akitokea Chelsea.
Jackson alisajiliwa na Chelsea kutoka Villarreal kwa Pauni 32 milioni mwaka 2023 lakini baada ya kuona hana nafasi kubwa ya kucheza aliomba kutolewa kwa mkopo kwenda Bayern katika dili lililokuwa karibu kuvunjika baada ya Chelsea kuiambia timu hiyo haina mpango wa kuendelea na mchakato, baada ya Liam Delap kuumia, hivyo walihitaji staa huyo arejee kuziba pengo lake.
Hata hivyo, Jackson aligoma na kusisitiza hatorudi na mwisho dili likafanyika.
Tangu kuanza kwa msimu huu Jackson ambaye mkataba wake na Chelsea unatarajiwa kumalizika mwaka 2033 amecheza mechi sita za michuano yote na hajaonekana kuwa katika kiwango bora lakini Kocha Vincent Kompany anaamini staa huyo atasaidia sana kwenye safu ya ushambuliaji siku za mbele.
Frenkie de Jong
MACHESTER United inaangalia uwezekano wa kumsajili kiungo wa Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi, Frenkie de Jong, mwenye umri wa miaka 28, dirisha lijalo. Hata hivyo, hivi karibuni taarifa zilidai Barca imefikia makubaliano ya kumsainisha mkataba mpya staa huyu na amekubali kupunguza mshahara wake. Mkataba wa De Jong unamalizika mwisho wa msimu huu na kwa muda mrefu Man United imekuwa ikiisaka saini yake.
Mike Maignan
CHELSEA ilijiondoa kwenye ushindani wa kumsajili kipa wa zamani Paris Saint-Germain, Gianluigi Donnarumma ambaye kwa sasa anaichezea Manchester City ili kuwekeza nguvu zaidi kwa kipa wa AC Milan, Mike Maignan ambaye pia ilishindwa kumpata baada ya kutofikia mwafaka katika masuala ya ada ya uhamisho. Kwa sasa Chelsea ambayo inaonekana kuwa upungufu katika eneo lao la kipa inataka kurudi tena mezani kuzungumza na Maignan.
Dayot Upamecano
LIVERPOOL inatarajia kumsajili beki wa kimataifa wa Ufaransa, Dayot Upamecano, mwenye umri wa miaka 26, mara tu mkataba wake na Bayern Munich utakapomalizika mwisho wa msimu huu. Katika mchakato huo pia wanaweza kukumbana na upinzani mzito kutoka Real Madrid ambayo pia inahitaji saini yake. Upamecano amecheza mechi zaidi ya mechi 130 na Bayern Munich tangu alipojiunga mwaka 2021.
Staa huyu anaonekana kama mbadala wa Konate.
Joao Palhinha
TOTTENHAM Hotspur inataka kumsajili moja kwa moja kiungo mkabaji wa Bayern Munich, Joao Palhinha, 30, baada ya kuvutiwa na kiwango alichoonyesha tangu kuanza kwa msimu huu. Palhinha alisajiliwa na Bayern dirisha la majira ya kiangazi mwaka jana kutoka Fulham kwa dau la takribani Euro 51 milioni na tangu atue Spurs amecheza mechi tisa za michuano yote na kufunga mabao mawili.
Ibrahima Konate
LIVEPROOL imeanza rasmi mazungumzo ya kumwongeza mkataba mpya beki wao wa kimataifa wa Ufaransa Ibrahima Konate, mwenye umri wa miaka 26, ambao ulitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Mara kadhaa ilidaiwa pia Madrid inatamani sana huduma yake na Konate mwenyewe anatamani sana kujiunga nayo, hivyo hatosaini mkataba mpya.
Takefusa Kubo
ARSENAL inataka kusajili wachezaji wawili wa Real Sociedad watakaoigharimu Euro 75 milioni kwa pamoja dirisha lijalo. Mastaa hao ni winga wa kimataifa wa Japani, Takefusa Kubo, 24, na beki kutoka Ufaransa Lucien Agoume, 23. Kubo, aliyewahi kuwa mali ya Real Madrid, ameng’ara sana La Liga akiwa na Sociedad tangu msimu uliopita.
Eduardo Camavinga
Newcastle United ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kiungo wa kimataifa wa Ufaransa, Eduardo Camavinga, 22, anayefikiria kuondoka Real Madrid mwisho wa msimu huu. Camavinga alisajiliwa na Madrid kutoka Rennes mwaka 2021 kwa Euro 31 milioni lakini hivi karibuni inadaiwa kuwasiliana na wawakilishi wake akitaka kuondoka kutafuta changamoto mpya sehemu nyingine.