Bayern Munich yautaka ubingwa wa Ulaya
Muktasari:
- Bayern ilianza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa kwa kishindo baada ya kuichapa Bodo/Glimt mabao 5-0, katika mchezo ambao kipindi cha kwanza kilimalizika bila timu hizo kufungana.
MUNICH, UJERUMANI: BAYERN Munich imeweka wazi azma yake ya kutwaa tena taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku nahodha Harry Kane akisema timu hiyo ipo katika hali ya “unyenyekevu na njaa” ya kufika mbali zaidi katika michuano hiyo.
Bayern ilianza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa kwa kishindo baada ya kuichapa Bodo/Glimt mabao 5-0, katika mchezo ambao kipindi cha kwanza kilimalizika bila timu hizo kufungana.
Kane alifunga bao moja, huku Michael Olise akifunga mawili na Jamal Musiala pamoja na Alphonso Davies wakiongeza mabao mengine.
Ushindi huo umeongeza matumaini ya Bayern kufanya vizuri katika msimu huu, baada ya klabu hiyo kukosa nafasi ya kufika fainali msimu uliopita.
Bayern ilifika hatua ya nusu fainali msimu uliopita, lakini ilitolewa na Paris Saint-Germain kwa jumla ya mabao 6-5.
Kane amesema uzoefu huo umewafanya wachezaji wa Bayern kuwa na hamu kubwa zaidi ya kufika hatua ya mwisho msimu huu.
“Ulikuwa msimu ambao tulikuwa karibu sana. Nusu fainali iliamuliwa na mambo madogo sana. Sasa tuna mwaka mwingine wa kufanya kazi na kocha na kuelewa mawazo yake. Tunaweza kuwa tishio kwa timu yoyote. Tuna unyenyekevu na njaa,” amesema Kane.
Bayern, ambayo imetwaa taji hilo mara sita na mara ya mwisho mwaka 2020, imefika nusu fainali mara mbili katika misimu mitatu iliyopita.
Kane pia ameendelea kuweka rekodi binafsi katika michuano hiyo. Mshambuliaji huyo amehusika moja kwa moja katika mabao 43 katika mechi 39 za Ligi ya Mabingwa akiwa na Bayern, akifunga mabao 34 na kutoa asisti tisa.
Pia amefunga katika mechi nane mfululizo za michuano hiyo, akifikia rekodi iliyowahi kufanywa na mastaa Cristiano Ronaldo, Robert Lewandowski na Ruud van Nistelrooy.
Kocha Vincent Kompany alisifu uvumilivu wa wachezaji wake baada ya kipindi cha kwanza ambacho Bayern ilitawala lakini ikashindwa kupata bao.
“Katika kipindi cha kwanza tulihitaji kuwa wavumilivu. Tulifunga kwa wakati sahihi kipindi cha pili, kisha mabao yakaja,” amesema Kompany.
Ushindi huo ulimfanya Kompany kufikisha ushindi wa 20 katika mechi 29 za Ligi ya Mabingwa akiwa kocha wa Bayern.
Bayern sasa imeanza safari yake ya kuwania taji la Ulaya ikiwa na matumaini makubwa ya kufika mbali na hatimaye kurejesha kombe hilo Allianz Arena.