Tunahitaji jezi mpya za AFCON 2027
Muktasari:
- Leo ni mwezi wa tisa, imebaki miezi mitatu tu mwaka huu umalizike ili tupindukie mwakani ambapo ndio mashindano hayo yatafanyika yakiandaliwa na sisi na ndugu zetu wa Kenya na Uganda.
KUNATAKIWA uwepo wa jezi mpya za Taifa Stars kwa ajili ya fainali AFCON mwakani zitakazofanyika hapa nchini na uzinduzi wake unatakiwa uwe mwaka huu.
Leo ni mwezi wa tisa, imebaki miezi mitatu tu mwaka huu umalizike ili tupindukie mwakani ambapo ndio mashindano hayo yatafanyika yakiandaliwa na sisi na ndugu zetu wa Kenya na Uganda.
Na imebaki kama miezi nane hivi kabla ya kufanyika kwa mashindano hayo kwa mara ya kwanza katika ardhi ya nchi yetu jambo ambalo ni historia kubwa na ya kipekee.
Sasa wakati wengine wanachakarika huko katika mambo mengine, anayehusika na jezi afanye mpango wa kutuletea toleo jipya la jezi za taifa Stars badala ya zile zinazotumika sasa.
Kwanza hizo jezi zenyewe za sasa zilizinduliwa zamani sana na zimetumika mfululizo bila wahusika kutuletea jezi mpya kama wanavyofanya nchi nyingine.
Na hizo jezi zitakazotumika na Taifa Stars kwenye AFCON mwakani hazitakiwi kuwa bora liende au funika kombe mwanaharamu apite kwa vile tu watu wana uhitaji na inaonekana watazinunua tu.
Ziwe zimebuniwa katika namna ambayo itawavutia watu kuzivaa huku zikibeba maana na thamani kubwa ambayo Taifa Stars itawakilisha kupitia mashindano hayo.
Hao wahusika wabuni kitu cha kueleweka na kama wanajijua hawawezi ni bora kuanzishwe hata mchakato maalum wa kuwapa watu fursa ya kubuni jezi hizo na kisha apatikane mshindi ambaye jezi yake ndio itatumika.
Nchi inavyoimba kuhusu AFCON ya mwakani, inatakiwa kila mmoja aunge mkono kwa kutimiza wajibu wake mahali alipo na mapema. Mfano ni hao wanaohusika na jezi.