Barcelona yaibwaga Chelsea ishu ya Dembele
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ripoti za Africafoot, mchezaji huyo anatarajiwa kuwasili Hispania katika siku chache zijazo ili kukamilisha usajili wake na klabu hiyo ya Catalonia.
BARCELONA, HISPANIA: KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Mali, Seydou Dembele anatarajiwa kusaini mkataba wa kuichezea Barcelona wakati wowote kuanzia sasa akitokea katika kituo cha kukuza vipaji cha Jean Marc Guillou Academy de Bamako maarufu kama JMG Academy Bamako nchini kwao.
Akiwa na umri wa miaka 18, Dembele mwenye kipaji kikubwa ambaye alikuwa karibu kujiunga na Chelsea, inaonekana amebadilisha uamuzi wake na sasa anatarajiwa kusaini mkataba wa kuichezea Barcelona huku suala la kikomo cha dili hilo kikiwa hakijawekwa wazi.
Kwa mujibu wa ripoti za Africafoot, mchezaji huyo anatarajiwa kuwasili Hispania katika siku chache zijazo ili kukamilisha usajili wake na klabu hiyo ya Catalonia.
Chelsea walikuwa tayari kulipa Euro 1.5 milioni kwa ajili ya kinda huyo, ambaye pia alikuwa akiwindwa na Red Bull Salzburg, klabu yenye uhusiano na Akademi ya JMG pamoja na Fenerbahce ya Uturuki.
Dembele, mwenye urefu wa futi 5.4 aling’ara katika michuano ya Kombe la Dunia la vijana chini ya miaka 17 iliyofanyika Qatar akiwa na timu ya taifa ya Mali U17, ambapo alifunga mabao mawili na kutoa asisti nne za mabao katika mechi tano.
Licha ya kimo chake kifupi, alionyesha kiwango cha juu akiwa anavaa namba 10 katika Akademi ya JMG akiwa na sifa ya wepesi, ubunifu mkubwa na uwezo mzuri wa kutoa pasi za kupasua safu ya ulinzi kwa kutumia mguu wake wa kushoto.
Katika michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon) chini U-17 iliyofanyika Morocco, Dembele alicheza mechi sita akifunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao.