Aziz Ki ana jambo lake na Man City leo

Muktasari:
- Ukiweka kando kipute hicho cha Man City na Wydad, mashabiki watapata uhondo mwingine, ambapo Real Madrid itakuwa na kasheshe zito mbele ya Al Hilal ya Saudi Arabia.
PHILADELPHIA, MAREKANI: MABEKI wa Manchester City watakabiliwa na shughuli pevu ya kumdhibiti Stephane Aziz Ki wa Wydad AC wakati miamba hiyo itakapokutana kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya fainali za Kombe la Dunia la Klabu utakaofanyika Lincoln Financial Field huko Philadelphia, Marekani, usiku wa leo Jumatano.
Ukiweka kando kipute hicho cha Man City na Wydad, mashabiki watapata uhondo mwingine, ambapo Real Madrid itakuwa na kasheshe zito mbele ya Al Hilal ya Saudi Arabia.
Usiku wa kuamkia leo, Jumatano ulishuhudia mechi nyingine mbili, ambapo Inter Milan ilikuwa bize kukipiga na Monterrey, wakati Ulsan Hyundai ilimalizana na Mamelodi Sundowns FC.
Man City na miamba ya Morocco, Wydad AC itakutana kwenye uwanja wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 67,594. lakini wasiwasi uliopo ni kama mashabiki watajitokeza wa kutosha kutokana na kile kilichotokea kwenye mechi ya Chelsea iliposhinda 2-0, ambapo mashabiki 22,137 walijitokeza kwenye uwanja wenye uwezo wa kuingiza mashabiki wanaoketi zaidi ya 71,000.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola anatazamiwa kuwapa nafasi mastaa wake watatu aliowasajili kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, Rayan Cherki, Rayan Ait-Nouri na Tijjani Reijnders ambapo kwa pamoja wakali hao wameigharimu miamba hiyo ya Etihad, Pauni 108 milioni.
Rekodi zinaonyesha kwamba Man City imepoteza mara moja tu katika mechi 13 za mwisho za mashindano. Lakini, Wydad, inayolewa nafasi ndogo ya kushinda mechi hiyo, inaamini inaweza kuleta ushindani mkali ndani ya uwanja kwa kuwa na huduma bora kabisa za wachezaji wake, akiwamo staa wa Burkina Faso, Aziz Ki, ambaye imemsajili kutoka Yanga ya Tanzania kwenye dirisha hili.
Man City na Wydad zimepangwa pamoja kwenye Kundi G pamoja na timu za Al Ain na Juventus, huku mashabiki wengi wakisubiri kwa hamu kuona mavitu ya Rayan Cherki, ambaye ni hodari kwa pasi za mabao.
KIKOSI CHOTE CHA WYDAD AC; Makipa: Omar Aqzdaou, El Mehdi Benabid, Youssef El Motie Mabeki: Abdelmounaim Boutouil, Ayoub Boucheta, Guilherme Ferreira, Jamal Harkass, Bart Meijers, Fahd Moufi, Mohamed Moufid
Viungo: Arthur, Stephane Aziz Ki, Ismail Benktib, Yassine Bennani, Rayane Mahtou, Mickael Malsa, El Mehdi El Moubarik, Ismail Moutarajji, Pedrinho, Oussama Zemraoui
Washambuliaji: Omar Alsomah, Nordin Amrabat, Zakaria Fathi, Hamza Hannouri, Thembinkosi Lorch, Cassius Mailula, Selemani Mwalimu, Samuel Obeng, Mohamed Rayhi.