Axel Tuanzebe aishtaki Man United
Muktasari:
- Tuanzebe, 27, ambaye kwa sasa anaichezea Burnley, amefungua kesi Mahakama Kuu kudai klabu yake hiyo ya zamani haikumpa ushauri sahihi wa kuhusu afya yake.
LONDON, ENGLAND: MAMBO ni moto. Manchester United imefunguliwa mashtaka na mchezaji wao wa zamani Axel Tuanzebe akiishutumu timu hiyo kushindwa kumpatia ripoti nzuri za kitabibu, imeelezwa.
Tuanzebe, 27, ambaye kwa sasa anaichezea Burnley, amefungua kesi Mahakama Kuu kudai klabu yake hiyo ya zamani haikumpa ushauri sahihi wa kuhusu afya yake.
Tuanzebe alijiunga na Man United alipokuwa na umri wa miaka minane na alikuwa nahodha wa timu zote za ngazi za vijana. Hata hivyo, aliondoka kwenye timu hiyo mwaka 2023 baada ya kupata majeraha mfululizo yaliyomtibulia kupata nafasi kwenye kikosi cha wakubwa, akiishia mechi 37 tu.
Ripoti ya gazeti la Telegraph inadai wanasheria wa Tuanzebe wamegoma kutoa maelezo yoyote ya kuhusu mashtaka hayo, ambayo yanadaiwa kufunguliwa mahakamani miaka miwili iliyopita wakati alipoachana na miamba hiyo ya Old Trafford. Man United nayo imeshindwa kueleza kitu baada ya kufuatwa na SunSport kwa ajili ya kutoa ufafanuzi.
Wakati akiwa Man United, Tuanzebe alitolewa kwa mkopo kwenye timu za Aston Villa, Napoli na Stoke.
Na licha ya kuonyesha kiwango kizuri kwenye baadhi ya mechi akiwa na Man United, ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Paris Saint-Germain, ambayo alimdhibiti kwelikweli Kylian Mbappe na wenzake, hakuwahi kuwa na uhakika wa namba kwenye kikosi hicho.
Lakini, misimu miwili akiwa na Tractor Boys, alionekana kucheza vizuri kuliko miaka yake saba aliyokuwa kwenye kikosi cha Man United, ambako aliondoka kwa uhamisho wa bure kabisa.
Ishu yake ya kiafya ilianza Oktoba 2019, wakati alipopata maumivu ya nyonga wakati akipasha misuli moto kwenye mechi ya sare ya bao 1-1 baina ya Man United na Liverpool.
Staa huyo wa zamani za vijana za England aliweka nje ya uwanja kwa msimu mzima baada ya kujiumiza kwenye mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Colchester. Maumivu ya msimu yalimfanya awe nje ya uwanja msimu uliofuatia.
Kisha alipata majeraha mengine ya muda mrefu mwanzoni mwa msimu wa 2023/24 na alishindwa kufanya mazoezi hadi Januari. Majeraha yamekuwa yakimwandama na kumpa wakati mgumu wa kuonyesha ubora wake ndani ya uwanja. Oktoba mwaka jana, Tuanzebe alijiumiza kidole gumba wakati anafua na hivyo kuhitaji kufanyiwa upasuaji.
Jambo hilo lilimfanya akose mechi nne, kabla ya kuumia misuli ambayo ilimweka nje ya uwanja kuanzia mwanzoni mwa Desemba hadi katikati ya Januari, kabla ya kukosa mechi mbili zaidi kutokana na kuvunja kidole gumba Machi mwaka huu.