Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Arteta: Dhamira yangu hainisuti kwa City

Muktasari:

  • Arteta alifanya kazi Manchester City kati ya mwaka 2016 na 2019, kipindi kinachogusa baadhi ya misimu tisa ambayo klabu hiyo imekutwa na hatia ya kukiuka kanuni za ligi na kuficha ufadhili wa zaidi ya pauni830 milioni.

LONDON, England: KOCHA Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema hana wasiwasi kuhusu dhamira yake kuhusiana na ukiukaji wa kanuni za Ligi Kuu England unaoikabili Manchester City, klabu aliyowahi kufanya kazi nayo kama kocha msaidizi wa Pep Guardiola.

Arteta alifanya kazi Manchester City kati ya mwaka 2016 na 2019, kipindi kinachogusa baadhi ya misimu tisa ambayo klabu hiyo imekutwa na hatia ya kukiuka kanuni za ligi na kuficha ufadhili wa zaidi ya pauni830 milioni.

Akizungumza kwa mara ya kwanza na waandishi wa habari tangu kutolewa kwa uamuzi huo, Arteta alijaribu kuepuka maswali kuhusu suala hilo, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu mchakato unaoendelea, kwa kuwa City imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Hata hivyo, alipoulizwa moja kwa moja kama dhamira yake iko safi kutokana na nafasi aliyokuwa nayo City, kocha huyo Mhispania alijibu kwa neno moja tu: “Ndiyo.”

Jibu hilo lilikuwa fupi, lakini lilikuwa miongoni mwa kauli zilizovutia zaidi katika mkutano huo na waandishi wa habari, ambao kwa sehemu kubwa Arteta alisisitiza kuwa hataki kutoa maoni kuhusu suala hilo hadi mchakato ukamilike.

Alipoulizwa kama amezungumza na Guardiola kuhusu sakata hilo, Arteta alisema: “Napendelea kutokujibu maswali hayo.”

Tume huru iliyochunguza tuhuma dhidi ya City ilibaini kuwa klabu hiyo ilipanga mikataba ya kibiashara isiyo halisi na baadhi ya washirika wake ili kuficha mapato yake.

Akizungumzia ripoti hiyo, Arteta alisema anaelewa maswali yanayoulizwa, lakini akaongeza kuwa ni muhimu kuheshimu utaratibu na muda wa kushughulikia suala hilo.

“Ninaelewa kabisa swali, lakini ni muhimu tuheshimu mchakato na muda wake. Bado suala hili halijafikia mwisho kwa sababu rufaa imewasilishwa,” alisema.

Aliongeza kuwa msimamo wake na wa Arsenal ni kutotoa maoni zaidi hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi wa mwisho.

Arteta pia aliulizwa kama anaona ni muhimu rufaa na adhabu zinazoweza kutolewa zikamilishwe ndani ya msimu huu ili kulinda uadilifu wa Ligi Kuu England.

Alijibu kuwa wenye jukumu la kusimamia mchakato huo wanapaswa kufikia uamuzi sahihi, akisisitiza kuwa wanaamini suala hilo litashughulikiwa ipasavyo.

Pamoja na sakata hilo, Arteta alisema anaamini kwa asilimia 100 kuwa Ligi Kuu England bado ndiyo ligi bora zaidi duniani.

Arsenal, ambayo ilikuwa nyuma ya vinara Manchester City kwa pointi tatu wakati wa taarifa hiyo, ilikuwa ikijiandaa kukabiliana na Leeds United, inayoshika nafasi ya tano, kwenye Uwanja wa Emirates jana.