Arteta ataka kumkumbatia refa, akapigwa kadi
Muktasari:
- Arteta anajulikana kwa kuwa kocha mwenye hisia kali akiwa kwenye eneo la benchi, mara kwa mara akijaribu kusukuma timu yake kupata matokeo huku akikaribia kuvuka mipaka ya eneo lake la ufundi.
SUNDERLAND, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta alijikuta kwenye tukio la kushangaza baada ya kupewa kadi ya njano katika mchezo dhidi ya Sunderland, lakini namna alivyojaribu kukwepa adhabu hiyo iliwachekesha mashabiki.
Arteta anajulikana kwa kuwa kocha mwenye hisia kali akiwa kwenye eneo la benchi, mara kwa mara akijaribu kusukuma timu yake kupata matokeo huku akikaribia kuvuka mipaka ya eneo lake la ufundi.
Jumamosi kwenye Uwanja wa Stadium of Light, ilionekana kama alifanya hivyo tena, jambo lililomfanya mwamuzi John Brooks amfuate mwishoni mwa kipindi cha kwanza ambacho kilimalizika bila bao.
Brooks alitumia kusimama kwa mchezo huo kumfuata Arteta ili kumwonya rasmi kwa kutoka nje ya eneo lake la ufundi. Lakini wakati mwamuzi huyo akielekea kwake huku akiingiza mkono mfukoni kuchukua kadi, Arteta alitabasamu na kujaribu kumkumbatia.
Hata hivyo, Brooks hakuitikia jaribio hilo. Arteta alisitisha mpango wake huo kabla ya mwamuzi kumwonyesha kadi ya njano na kumwandika kwenye daftari.
Tabasamu la Arteta lilitoweka ghafla baada ya kuona kadi hiyo, huku akionekana kushangazwa na adhabu aliyopewa. Alianza kumweleza Brooks kwa hasira, uso wake ukibadilika kutoka tabasamu hadi kukunjamana.
Tukio hilo lilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na kuwachekesha mashabiki.
Shabiki mmoja aliandika: “Alijaribu kumkumbatia, lakini akapuuzwa.”
Mwingine akaandika kwa utani: “Alijaribu kwenda kumbusu.”
Arteta alizidi kukerwa na uamuzi wa waamuzi kipindi cha pili baada ya Sunderland kupewa penalti kufuatia mzozo wa kugusana kwa wachezaji wakati wakisubiri mpira wa kona.
Hata hivyo, kipa wa Arsenal, David Raya aliokoa penalti hiyo kwa ustadi mkubwa na kuwaokoa wageni.
Dakika chache baadaye, Bruno Guimaraes aliipatia Arsenal bao la kuongoza kwa shuti kali la mbali, akibadilisha kabisa hali ya mchezo.