Arsenal yaajiri kampuni kutafuta makombe
Muktasari:
- Arsenal ilitwaa taji la Ligi Kuu msimu uliopita, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2004, na sasa viongozi wa klabu hiyo wanataka kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelea kwa muda mrefu.
LONDON, ENGLAND: Mabingwa wa Ligi Kuu England, Arsenal, wameajiri kampuni ya ushauri kutoka Marekani kufanya tathmini ya namna klabu hiyo inaweza kuendeleza mafanikio yake kwa mfumo endelevu baada ya kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 22.
Arsenal ilitwaa taji la Ligi Kuu msimu uliopita, ikiwa ni mara ya kwanza tangu mwaka 2004, na sasa viongozi wa klabu hiyo wanataka kuhakikisha mafanikio hayo yanaendelea kwa muda mrefu.
Kampuni ya ushauri ya Marekani, BCG, imepewa jukumu la kufanya tathmini hiyo, ambayo itachunguza maeneo mbalimbali ya uendeshaji wa klabu na namna ya kuhakikisha Arsenal inaendelea kuwa na mafanikio ndani na nje ya uwanja.
Kama ilivyo kwa tathmini nyingine za kifedha, kuna uwezekano wa klabu kupunguza baadhi ya gharama au kuelekeza uwekezaji katika maeneo mengine.
Hata hivyo, hakuna uamuzi wowote ambao umefanywa hadi sasa kutokana na tathmini hiyo.
Msimu uliopita ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Arsenal chini ya Mikel Arteta. Mbali na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, timu hiyo pia ilifika fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la Ligi.
Licha ya klabu hiyo kuvunja rekodi yake ya mapato katika ripoti yake ya hivi karibuni ya kifedha, Arsenal imekuwa ikipata hasara katika kipindi cha miaka saba iliyopita.
Mafanikio ya msimu uliopita yameongeza mapato kupitia zawadi za mashindano pamoja na matarajio ya kupata mikataba mipya ya kibiashara, lakini pia yamekuja na gharama kubwa.
Wachezaji na wafanyakazi walitarajiwa kupata bonasi kubwa baada ya kutwaa ubingwa, huku klabu pia ikitakiwa kugharamia shughuli mbalimbali za sherehe za ubingwa, ikiwamo gwaride la kombe.
Moja ya maeneo ambayo Arsenal imefanya vizuri kwa miaka ya karibuni ni biashara. Klabu hiyo iliripoti mapato ya kibiashara ya pauni 263.2 milioni katika hesabu zake za hivi karibuni, kutoka pauni 218.3 milioni mwaka uliotangulia.
Kwa sasa Arsenal ina zaidi ya washirika 30 wa kibiashara, wakiwamo Coca-Cola, Guinness, Facebook na Paramount.
Mapato ya biashara ya rejareja nayo yaliongezeka kwa asilimia 27 mwaka uliopita, huku uzinduzi wa jezi mpya na bidhaa mbalimbali za klabu kwa kushirikiana na Adidas ukichangia ongezeko hilo.
Hata hivyo, Arsenal imepata pigo baada ya Afisa Mkuu wa Biashara wa klabu hiyo, Juliet Slot, ambaye alikuwa sehemu muhimu ya mafanikio hayo ya kibiashara, kuondoka katika nafasi yake msimu huu.
Sasa viongozi wa Arsenal wanataka tathmini hiyo kusaidia kuhakikisha mafanikio ya Arteta na timu yake hayaishii kuwa mafanikio ya muda mfupi, bali yanajengwa katika mfumo utakaoiweka klabu hiyo kileleni kwa miaka ijayo.