Arteta aongeza mingine Arsenal hadi 2030
Muktasari:
- Arteta, aliyejiunga na Arsenal mwezi Desemba 2019, aliiongoza timu hiyo kushinda taji lake la kwanza la Ligi Kuu England baada ya miaka 22 msimu uliopita, na hivyo kutwaa ubingwa wa 14 wa Ligi ya Kuu England.
Mikel Arteta amesaini mkataba mpya wa muda mrefu na Arsenal, akiongeza muda wake wa kuendelea kuwa kocha wa timu hiyo hadi Juni 2030.
Arteta, aliyejiunga na Arsenal mwezi Desemba 2019, aliiongoza timu hiyo kushinda taji lake la kwanza la Ligi Kuu England baada ya miaka 22 msimu uliopita, na hivyo kutwaa ubingwa wa 14 wa Ligi ya Kuu England.
Mhispania huyo ameiongoza Arsenal katika michezo 361 kwenye mashindano yote, akiwa na kiwango cha ushindi cha asilimia 62.05, ambacho ndicho cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa na kocha yeyote aliyewahi kuhudumu katika historia ya Arsenal.
Arteta amesema anajivunia kuendelea kuiongoza klabu hiyo na anaamini mafanikio ya hivi karibuni ya Arsenal ni mwanzo tu.
“Ni heshima kubwa kuendelea na safari yangu katika klabu hii na kuendelea kufanya kazi na watu bora ambao wanaitakia Arsenal mema,” alisema Arteta.
“Arsenal ni klabu ya kipekee, ina tabia yake na namna ya kukufanya ujisikie, na ninajiona mwenye bahati kubwa kwamba safari yetu pamoja itaendelea.”
Aliongeza: “Tayari tumejenga uhusiano wa kipekee na kuunda kumbukumbu zitakazodumu maisha yote. Kinachosisimua zaidi ni kwamba huu ni mwanzo tu wa kile tunachoweza kukifanikisha pamoja.”
Arteta pia aliwashukuru wamiliki wa Arsenal na mashabiki kwa imani na sapoti yao ya kuendelea, akielezea mkataba huo mpya kama wakati wa kujivunia kwake pamoja na familia yake.
Wafanyakazi wake wa benchi la ufundi pia wamekubali kusaini mikataba mipya itakayodumu kwa muda kama wa Arteta, hadi Juni 2030.