Arsenal yawekwa pembeni ubingwa
Muktasari:
- Merson alibadili utabiri wake baada ya kile alichokiona kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili. Liverpool ilionekana kuwa washindi kwenye dirisha la usajili la majira ya kiangazi la mwaka huu, wakati mabingwa hao wa Ligi Kuu England waliponasa saini za Hugo Ekitike, Florian Wirtz, Milos Kerkez na Jeremie Frimpong kabla ya kufunga dirisha hilo kwa usajili wa straika wa Newcastle United, Alexander Isak, aliyenaswa kwa ada ya Pauni 130 milioni.
LONDON, ENGLAND: STAA wa zamani wa Arsenal, Paul Merson, amesema sasa amebadili utabiri wake kwamba timu yake hiyo ya zamani itabeba taji la Ligi Kuu England msimu huu na badala yake, anawataja Liverpool ndio watakaokuwa wababe.
Merson alibadili utabiri wake baada ya kile alichokiona kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili. Liverpool ilionekana kuwa washindi kwenye dirisha la usajili la majira ya kiangazi la mwaka huu, wakati mabingwa hao wa Ligi Kuu England waliponasa saini za Hugo Ekitike, Florian Wirtz, Milos Kerkez na Jeremie Frimpong kabla ya kufunga dirisha hilo kwa usajili wa straika wa Newcastle United, Alexander Isak, aliyenaswa kwa ada ya Pauni 130 milioni.
Kabla ya msimu kuanza, Merson aliipa nafasi Arsenal kumaliza ukame wao wa kushinda taji la Ligi Kuu England msimu huu. Lakini, sasa msimamo huo umebadilika baada ya usajili uliofanywa na Liverpool kuonekana kama ni timu iliyopania kunyakua taji hilo.
Alipoulizwa kama Liverpool sasa inaweza kushinda taji la Ligi Kuu England, staa huyo wa zamani wa kimataifa wa England, alisema: “Ndio, ninaamini hilo baada ya kuona kilichotokea.
“Baada ya kumsajili Isak. Unaweza kuona kabisa hawa watu wanataka ubingwa. Mwanzoni nilidhani Arsenal ina faina kubwa baada ya kushinda dhidi ya Man United, lakini sasa kila kitu kimebadilika ghafla baada ya Liverpool kuzishinda Newcastle na Arsenal.”
Liverpool ilimtaka pia beki wa kati Marc Guehi kabla ya kumkosa kwenye dakika za mwisho kabisa, usajili ambao ungekifanya kikosi hicho cha Arne Slot kuwa tishio zaidi uwanjani.
Liverpool mechi yao ijayo baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kimataifa itakipiga na Burnley kwenye Ligi Kuu England, kisha itahamia kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambako itacheza na Atletico Madrid na baada ya hapo ni Merseyside derby dhidi ya Everton uwanjani Anfield, Septemba 20.