Arsenal yamnyakua Guimaraes
Muktasari:
- Guimaraes, 28, ambaye alikuwa nahodha wa Newcastle, amesaini mkataba wa miaka minne na Arsenal wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja, katika usajili unaoonekana kuwa moja ya hatua kubwa za mabingwa hao wa Ligi Kuu England katika dirisha hili.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imekamilisha usajili wa kiungo wa kimataifa wa Brazil, Bruno Guimaraes, kutoka Newcastle United kwa ada ya Pauni 75 milioni, sawa na zaidi ya Sh250 bilioni za Tanzania.
Guimaraes, 28, ambaye alikuwa nahodha wa Newcastle, amesaini mkataba wa miaka minne na Arsenal wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja, katika usajili unaoonekana kuwa moja ya hatua kubwa za mabingwa hao wa Ligi Kuu England katika dirisha hili.
Kiungo huyo alikuwa ameweka wazi mapema alitamani kujiunga na Arsenal, licha ya kuwa na historia kubwa na Newcastle tangu alipowasili klabuni hapo mwaka 2022.
Guimaraes amesema uamuzi wa kuondoka Newcastle ulikuwa miongoni mwa uamuzi magumu zaidi aliyowahi kuyafanya kutokana na uhusiano mkubwa alioujenga na klabu hiyo.
“Uamuzi huu ni mgumu kwa sababu Newcastle ina maana kubwa kwangu. Lakini nilitaka kupata uzoefu mpya katika maisha yangu. Nahisi niko tayari kwa changamoto mpya kwa ajili yangu na familia yangu,” amesema.
Ameongeza kuwa sasa yupo tayari kuanza ukurasa mpya wa maisha yake ya soka, huku akisisitiza kwamba lengo lake ni kushinda mataji akiwa Arsenal.
“Niko kwenye hatua ya maisha yangu ambayo nahitaji changamoto kama hii. Nataka kushinda mataji, nataka kuweka historia na naamini nimefika sehemu sahihi kufanya hivyo.”
Guimaraes aliondoka kwenye kambi ya Newcastle iliyokuwa La Manga, Hispania, mapema wiki hii ili kukamilisha uhamisho wake kwenda Uwanja wa Emirates baada ya klabu hizo kufikia mwafaka katika mazungumzo.
Kabla hata hajaanza mazoezi na kikosi chake kipya, Guimaraes alifichua kwamba tayari amepokea jumbe kutoka kwa baadhi ya wachezaji wa Arsenal, akiwemo nyota mwenzake wa Brazil, Gabriel, pamoja na kiungo Declan Rice.
Guimaraes na Rice wamewahi kukutana mara kadhaa kwenye mapambano ya ligi wakiwa viungo wa timu pinzani, lakini sasa watakuwa upande mmoja.
Rice alimtumia ujumbe wa kumkaribisha kwa utani akisema: “Njoo hapa na tafadhali hakuna tena mapambano, sasa sisi ni marafiki.”
Guimaraes alijiunga na Newcastle Januari 2022 wakati klabu hiyo ikiwa katika hatari ya kushuka daraja, lakini akawa sehemu muhimu ya mabadiliko makubwa ya timu hiyo chini ya kocha wa zamani Eddie Howe.
Baada ya muda mfupi, Mbrazil huyo aligeuka kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi wa Newcastle na baadaye akapewa jukumu la unahodha.
Historia yake kubwa zaidi Newcastle ilikuja mwaka 2025 alipoiongoza timu hiyo kutwaa Kombe la Carabao baada ya kuifunga Liverpool katika fainali.
Ushindi huo ulimfanya Guimaraes kuwa nahodha wa kwanza wa Newcastle kwa takribani miaka 70 kunyanyua kombe kubwa la ndani.
Pia, alikuwa sehemu ya kikosi kilichoiwezesha Newcastle kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2023 na tena mwaka 2025.
Hata hivyo, Newcastle ilipitia msimu mgumu uliopita baada ya kumaliza nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Sasa Guimaraes ameacha St James' Park na kujiunga na Arsenal akiwa na matarajio makubwa ya kuongeza ubora wa safu ya kiungo na kusaidia klabu hiyo kupigania mataji ya ndani na Ulaya.
Kwa Arsenal, usajili huo unaongeza nguvu katika kikosi kinacholenga kuendelea kutawala soka la England na kufanya vizuri zaidi katika michuano ya Ulaya.